Serikali inathamini jitihada za wadau katika kuhifadhi, kutunza na kusambaza lugha za makabila mbalimbali nchini ambazo ndio msingi wa lugha aushi ya Kiswahili ambayo ni lugha ya taifa.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaam na Mhariri Mkuu wa Bazara la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Richard Mtambi alipokuwa akisoma hotuba ya Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Historian a Mila za Kabila la Wasukuma, Wasilanga wa Nasa wa mkoani Simiyu.

Akisoma hotuba ya Katibu Mkuu huyo, Mtambi alisema kuwa mwandishi wa kitabu hicho pamoja na ushirikiano wa Wasilanga wa Nasa wameongeza hazina kubwa kwa taifa ya kukusanya, kuhifaadhi na kusambaza mila na desturi za moja ya makabila zaidi ya 120 ya Tanzania.

Katika hotuba hiyo, Profesa Gabriel amewaasa makabila mengine nchini waige mfano wa Wasukuma wa Nasa wa kutunza na kuhifadhi mila na desturi zao kwa manufaa ya taifa ili kuhakikisha utamaduni wa Mtanzania unatunzwa, kuhifadhiwa na kuendelezwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha, Mkambi amesema kuwa BAKITA inathamini juhudi zinazofanywa na makabila mbalimbali nchini za kuhifadhi lugha zao maana lugha hizo zinasaidia kutengeneza na kuendeleza misamiati ya Kiswahili.

Kwa upande wake Mtemi wa Masanza, Magu Mkoani Mwanza Frederick Ntobi amesema uzinduzi wa kitabu hicho umekuwa chachu kwa utamaduni wa kuhifadhi historia, masimulizi, mafundisho na elimu mbalimbali katika kuendeleza utamaduni wa Mtanzania.

Ntobi ameyataja mambo ya msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika kuendeleza utamaduni wa Mtanzania yakiwemo kukusanya vitu vya kale na kusaidia kutunza kumbukumbu vitu vilivyofanyika wakati uliopita kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo ili kusaidia kutunza historia kwa wakiongozwa na uzalendo miongoni mwa jamii na taifa, na amewaonya watu wasiwe na tamaa ya kuuza kumbukumbu hizo kwa watu wa nje kwa maslahi binafsi.

Ntobi ameongeza kuwa mambo mengine ya kuzingatia katika kuendeleza utamaduni ni kutunza sanaa za kijadi ikiwemo michoro, mapishi ya kiasili ambayo yana manufaa kwa afya za walaji kwa kuhusisha siku ya kujifunza namna bora mapishi, kutunza maeneo ya matambiko ya kimila, kutunza lugha za asili pamoja na kutunza Ikulu za Kimila hatua ambayo itasaidia kukuza uchumi wa jamii husika na kuwa vyanzo vya mapato kwa Serikali.

Kuhusu Sera ya Taifa ya Utamaduni, Ntobi amesema kuwa Umoja wa Machifu nchini wapo tayari kutoa maoni yao ili waweze kusaidia kupatikana Sera bora kwa manufaa ya taifa na kuifanya sekta ya utamaduni iweze kuchangia katika pato la taifa kwa njia ya utalii na kukuza uchumi wa nchi.

Naye mtunzi wa kitabu hicho Mratibu wa Mila na Desturi wa Nasa Busega Johnson Rollas Gervas ameishukuru Serikali kwa kutahamini na kuunga mkono juhudi za kuhifadhi utamaduni kwa kuzingatia mila na desturi ambazo ndio utambulisho wa taifa.

Katika kuhakikisha amani ya nchi inaendelea kudumishwa, Johnson amesema kuwa watatumia ngoma, nyimbo na matamasha ambayo ni moja ya kazi ya sanaa ili kuweza kuunga juhudi za Serikali ya Awamu wa Tano kwa kushirikiana na Waziri mwenye dhamana ya utamaduni Mhe. Nape Nnauye na kuahidi kuwa wapo mstari wa mbele katika kuimarisha na kusimamia utamaduni wa Mtanzania.

Akitoa neno la shukrani kwa Mgeni Rasmi mara baada ya uzinduzi wa kitabu hicho, Felister Mayala Bwana amesema kuwa Busega wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kusimamia na kuendeleza utamaduni kwa kujenga na kuboresha kituo cha mila na desturi cha jamii ya kabila la Wasukuma wa Busega ili kuendelea kuitangaza Tanzania miongoni mwa mataifa kupitia sekta ya utamaduni.

Mwanadiplomasia Atoa Ushauli Kwa Vyama Vya Siasa,Asema hakuna Haja Ya Maandamano
Chadema Wakanusha Kuhusu Video Zinazozagaa Mitandaoni,Zikionyesha Maandalizi Ya Septemba 1