Mhariri wa gazeti la The Guardian linalomilikiwa na kampuni ya IPP Media Limited, Finnigan Simbeye ameokotwa leo katika eneo la Bunju wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam akiwa hajitambui.

Mke wa mhariri huyo, Rose Mirondo amesema kuwa alipata taarifa mapema asubuhi kuwa mumewe ameokotwa, alifika eneo hilo na kuambiwa na mashuhuda kuwa alichukuliwa na askari wa jeshi la polisi kwa ajili ya kumpeleka hospitalini.

Bi. Mirondo alisema kuwa mumewe aliondoka nyumbani Jumamosi ya Aprili 7 akiwa na gari na hakurejea hadi leo alipopata taarifa kuwa ameokotwa. Amesema kuwa alipofika eneo la tukio hakuliona pia gari la mumewe.

Mwanamke huyo ameongeza kuwa bado hajafahamu ni hospitali gani aliyopelekwa mumewe lakini anaelekea katika kituo cha polisi kwa lengo la kupata taarifa.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Murilo Jumanne amesema kuwa bado hajapata taarifa za kuokotwa kwa Simbeye.

Picha zilizosambaa mitandaoni zinaonesha kitambulisho cha kazi cha Simbeye.

Musiba awavaa TEF, awataka kutotumika kisiasa
Mahakama yaitaka Serikali kuhakikisha Miguna anafika mahakamani

Comments

comments