Kiungo wa klabu ya Man Utd Michael Carrick ataanza katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo kitakachocheza mchezo wa mwisho wa msimu huu dhidi ya Watford siku ya Jumapili katika uwanja wa Old Trafford.

Carrick mwenye umri wa miaka 36 ataanzishwa kwenye mpambano huo, ikiwa ni kusudio la kumpa heshima za mwisho kabla ya kustaafu soka rasmi.

Kiungo huyo aliejiunga na Man Utd mwaka 2006 akitokea Tottenham Hotspurs, tayari ameshaitumikia klabu hiyo inayojulikana kwa jina la utani la Mashetani Wekundu, katika michezo 463, alithibitisha kustaafu soka mwishoni mwa msimu huu, alipozungumza na waandishi wa habari mwezi March.

Meneja wa Man Utd Jose Mourinho amesema anatarajia kumuaga kwa heshima Carrick, na anaamini ataitumia nafasi ya kucheza mchezo huo dhidi ya Watford kwa kujiamini.

Mourinho amesema mbali na kumpa heshima hiyo, pia anatarajia kutoa nafasi ya kipekee kwa Carrick ya kuendelea kusalia klabuni hapo na kuwa kocha wa timu za vijana.

“Tunaamini atajiendeleza na baadae kuwa kocha wa moja ya vikosi vyetu vya vijana “.

“Kwa sasa mwili wake umedhihirisha hauwezi kuendelea kucheza soka, uongozi wa klabu na mimi binafsi tunahitaji kuuenzi mchango wake akiwa hapa Old Trafford,” Amesema meneja huyo kutoka nchini Ureno.

Carrick amefanikiwa kutwaa mataji matano ya ligi ya England akiwa na Man Utd na taji moja la ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Amefikia hatua ya kuwa nahodha wa kikosi cha Man Utd, baada ya kuondoka kwa Wayne Rooney mwishoni mwa msimu uliopita, lakini kwa bahati mbaya hakuweza kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kkosi cha kwanza.

“Ataanza katika kikosi cha kwanza mwishoni mwa juma hili tutakapocheza dhidi ya Watford hapa hapa Old Trafford, tutamrejeshea jukumu lake la unahodha siku hiyo, ili tumuage kwa heshima,” ameongeza Mourinho.

“Jambo kubwa ni uwezo na viwango alivyovionyesha akiwa hapa kwa zaidi ya miaka kumi, hatuna budi kurejesha fadhila ya kumpa heshima siku hiyo, ili tuionyeshe jamii tunamjali.”

Katika hatua nyingine Mourinho ana matumaini ya kumuona mshambuliaji Romelu Lukaku akirejea katika mchezo wa fainali wa kombe la chama cha soka England (FA CUP) utakaowakutanisha na Chelsea Mei 19.

Tayari imeshafahamika kuwa, mshambuliaji huyo kutoka nchini Ubelgiji atakosa michezo miwili ya mwisho ya ligi msimu huu, kufuatia majeraha ya kufundo cha mguu alioyapata wakati wa mpambano wa ligi dhidi ya Arsenal uliochezezwa Mei 06.

Kikosi cha Manchester Utd kesho kitasafiri kuelekea jijini London tayari kwa mchezo wa ligi dhidi ya West Ham Utd, na mwishoni mwa juma kitakua nyumbani Old Trafford kupapatuana na Watford.

Video: Kauli ya serikali kuhusu sakata la mafuta ya kupikia
Mwadini Ally awazidi kete Sure Boy, Frank Domayo