Mlinda mlango Michel Vorm amerejeshwa kwenye kikosi cha Tottenham, baada ya kuachwa mwishoni mwa msimu uliopita, kufuatia mkataba wake na klabu hiyo kufikia kikomo.

Vorm amerudi klabuni hapo kwa mkataba maalum, na ananatarajiwa kuwa langoni mwishoni mwa juma hili katika mchezo wa ligi kuu ya England dhidi ya Watford.

Vorm raia wa Uholanzi, amepewa nafasi hiyo, kufuatia kuumia kwa mlinda mlango chaguo la kwanza Hugo Lloris, alipokua kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Brighton.

Meneja wa Spurs Mauricio Pochettino amependekeza kurejeshwa kwa mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 35, ili asaidiane na Paulo Gazzaniga ambaye alikua chaguo la pili baada ya Lloris.

“Sijaona tofauti kubwa kurejea hapa, klabu hii ni kama nyumbani na ninaahidi kupambana ili kusaidia kufikia malengo,” alisema Vorm baada ya kukamilisha usajili wake akiwa kama mchezaji huru. “Nilipigiwa simu ya kunitaka kurudi hapa, na mimi sikukataa kufanya hivyo kwa sababu ninahitaji kuwa sehemu ya mafanikio ya klabu hii.”

“Tunahitaji kushikamana kwa pamoja, kila mmoja atambue mchango wa mwingine ili kufikia lengo,” aliongeza Vorm, ambaye amesisitiza kuwa tayari kwa mapambano ya kuwania nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Spurs.

Vorm atavaa jezi namba 13, ambayo aliitumia wakati akiwa klabuni hapo, kabla ya kuondoka mwishoni mwa msimu uliopita

Kwa mara ya kwanza Vorm alisajiliwa klabuni hapo mwaka 2014, na alifanikiwa kucheza michezo 47.

Mwakinyo atamba kumchakaza Mfilipino
Msumbuji yajitosa uchaguzi mkuu baada ya mkataba na waasi