Ligi Kuu ya soka pamoja na michezo mingine yote iliyosimamishwa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona, itarejea uwanjani kuanzia Juni mosi, ikiwa ni siku kumi kuanzia leo.

Ligi Kuu ilisimamishwa Mach 17, siku moja baada ya Serikali ya Tanzania kutangaza mtu wa kwanza kugundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo ulioua zaidi ya watu 320,000 kote duniani na kuambukiza zaidi ya watu milioni 4.1.

Ligi kuu ilisimamishwa wakati mabingwa watetezi Simba wakiongoza kwa zaidi ya pointi 17 juu ya Azam inayoshika nafasi ya pili, huku Young Africans ikiwa pointi moja chini.

Rais John Magufuli ametangaza uamuzi huo leo jijini Dodoma baada ya kumuapisha Godwin Mollel kuwa naibu waziri wa afya kushika nafasi ya Dk Faustine Ndungulile ambaye uteuzi wake ulitenguliwa. Pia aliapisha mabalozi na katibu tawala mmoja katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Alisema hali ya maambukizi imepungua na wagonjwa hospitalini wamepungua na hivyo kuamua kuruhusu michezo, kufungua vyuo na shule za elimu ya juu ya sekondari ambako wanafunzi wa kidato cha sita wsalikuwa wamebakiza mwezi mmoja kabla ya kuanza mitihani yao ya Taifa Mei 4.

“Mungu amesikia maombi yetu, tena amesikia kweli,” alisema Rais Magufuli.

“Hakuna Taifa ambalo linamtegemea Mungu halafu likashindwa.”

Ligi Kuu ya soka, mchezo wenye mashabiki wengi nchini, inatarajiwa akurejea bila ya mashabiki kuruhusiwa kuingia viwanjani, kwa mujibu wa rais wa Shirikisho la Soka (TFF), Wallace Karia aliyoitoa wakati michezo iliposimamishwa.

TARURA yarekebisha madaraja yaliyosombwa na mvua, Dodoma, Manyara
Picha ya zamani ya Rais yamtia mbaroni Idriss Sultan

Comments

comments