Mwanaharakati na mwanasiasa wa Kenya, Miguna Miguna ambaye alifukuzwa nchini humo na kupelekwa nchini Canada kwa nguvu ameibuka na kusema kuwa ataendelea kupinga utawala wa Uhuru Kenyatta ambao hauheshimu Katiba na sheria za nchi hiyo.

Ameyasema hayo wakati wa mahojiano na idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika, ambapo Miguna amesema kuwa mawakili wake tayari walikuwa wamewasilisha kesi katika mahakama moja jijini Nairobi kushinikiza serikali ya nchi hiyo kurejesha cheti chake cha kusafiria na vile vile kumruhusu kuingia nchini humo.

Amesema kuwa hatapumzika hadi pale serikali ya Uhuru Kenyatta itakapokubali kuwa imeingia madarakani kwa njia za udanganyifu.

“Hatutakubali, tutamlazimisha Uhuru kuheshimu katiba, ni lazima aamue kama anataka kuongoza kwa mujibu wa katiba au la,” amesema Miguna akiwa nyumbani kwake Richmond Hill, Ontario, Canada

Hata hivyo, Miguna aliwasili nchini Canada Jumatano usiku baada ya kufukuzwa nchini Kenya, ambako alikuwa anakabiliwa shtaka la uhaini.

Nape ang'ata na kupuliza usalama wa taifa
Makamu wa Rais wa Marekani amkwepa kiongozi wa Korea Kaskazini mezani