Vilio na majonzi vimetawala katika uwanja wa Nyamagana ambapo miili ya waandishi wa habari 5 pamoja na dereva aliekua akiendesha gari hilo inaagwa hii leo.

Baadhi ya waombolezaji katika uwanja wa Nyamagana

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameongoza zoezi la kuaga miili ya waandishi wa habari watano na dereva wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza waliofariki dunia katika ajali ya gari jana Januari 11.

Mhe. Nape Nnauye akiweka sahihi katika kitabu cha maombolezo uwanja wa Nyamagana

Miili ya marehemu hao baada ya kuagwa baadhi watafirishwa kwenda Arusha, Dar es Salaam, Kilimanjaro na mwingine ambao ni wa Husna Mlanzi wa ITV kuzikwa leo katika makaburi ya Kirumba jijini Mwanza.

Watakaosafirishwa kwenda Dar es Salaam ni Maofisa Habari wa Serikali Ngapemba na Msengi wakati Johari Shani wa Uhuru Digital atasafirishwa kwenda mkoani Arusha huku mwili wa Anthony Chuwa wa habari leo Digital utasafirishwa kwenda mkoa wa Kilimanjaro.

Waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea eneo la Shimanywile Wilaya ya Busega mkoani Mwanza baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso ni Johari Shani (Uhuru Digital), Husna Mlanzi (ITV), Anthony Chuwa (Habari Leo Digital), Abel Ngapemba (Ofisa Habari Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mwanza) na Steven Msengi aliyekuwa Ofisa Habari Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe.

Dereva wa gari la Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza walilopanda wanahabari hao, Paulo Silanga naye alifariki dunia na anatarajiwa kuagwa leo.

Hapo jana Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu lilisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi ambapo Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Blasius Chatanda alisema kabla ya ajali hiyo kutokea gari iliyokuwa imebeba waandishi wa habari iligonga lori aina ya Tata na kupoteza uelekeo kisha kuparamia dalalada iliyokuwa nyuma ikitokea mkoani Simiyu kwenda jijini Mwanza.

Matukio katika picha sherehe za Mapinduzi
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Januari 12, 2022