Madaktari bingwa 38 kutoka nchini China leo wameanza kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali kwa wananchi wa mikoa mitano nchini Tanzania.

Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo (Ijumaa, Julai 15, 2016) Katibu Mkuu wa Chama cha Urafiki kati ya Serikali ya Tanzania na China, Bw. Joseph Kahama alisema huduma ya matibabu na dawa zitatolewa bure.

Bw. Kahama amesema madaktari hao wanaofadhiliwa na Serikali ya China wameanza kutoa huduma katika mikoa ya Dodoma (6), Mara (5), Dar es Salaam (9), Tabora (5) na Lindi (6).

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Dk. Japhet Simeo ambaye amewapokea madaktari sita ambao leo wameanza kutoa huduma katika wilaya hiyo alisema watasaidia kutoa fursa kwa wananchi wenye matatizo sugu kupatiwa ufumbuzi.

“Madaktari niliowapokea ni pamoja na bingwa wa magonjwa ya watoto, upasuaji wa moyo, kisukari, shinikizo la damu, mifupa, macho, koo na masikio,” amesema.

Dk. Simeo amesema mbali na kuhudumia wananchi pia madaktari hao watasaidia kuboresha taarifa za aina ya magonjwa yanayowakabili wananchi wa wilaya hiyo.

“Kupitia madaktari hawa hospitali yetu ya wilaya itaboreshewa huduma katika baadhi ya maeneo kutokana na mapungufu yatakayojitokeza wakati wakiwahudumia wananchi ili kuboresha ufanisi wa kazi,” alisema.

Kwa Upande wake Waziri Mkuu aliwaomba wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi ili waweze kufanyiwa uchunguzi wa afya zao na kupatiwa matibabu na dawa kwa watakaogundulika na maradhi.

Amesema afurahishwa na mpango huo  unaoratibiwa na Chama cha  Urafiki kati ya Serikali ya Tanzania na China kwa kupeleka madaktari bingwa katika mikoa mbalimbali nchini kwa kuwa unatoa fursa kwa wananchi kujua afya zao.

Cristiano Ronaldo Ampeleka Luis Nani Hispania
Neven Subotic Anuakia Riverside Stadium