Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema misitu ya mikoko na majani ya baharini inatarajiwa kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa buluu kwa kuhifadhi hewa ya ukaa mara tano zaidi ya misitu ya kawaida.

Masanja amesema hayo, wakati akifungua warsha ya siku mbili ya wadau wa uhifadhi mfumo wa ikolojia wa hewa ya ukaa ya buluu na uendelezaji wa uchumi wa buluu Tanzania, lengo ikiwa ni kujadili namna bora ya kuondokana na changamoto zinazoikabili sekta ya misitu nchini.

Warsha hiyo, imefunguliwa Septemba 27,2022 katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam na ameelekeza washiriki wa warsha hiyo kuibua masuala muhimu yatakayoisaidia Serikali kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya biashara ya hewa ya ukaa.

Mikoko.

Amezitaja faida nyingine za misitu ya mikoko, kuwa ni kusaidia kukabiliana na athari za kimazingira kama mabadiliko ya tabia ya nchi, mmomonyoko wa udongo na vimbunga baharini, kusaidia uwepo wa mazalia ya samaki, chanzo cha kuni, mbao na milunda ya kujengea.

Aidha, amesema uwepo wa shughuli za kibinadamu katika misitu ya mikoko, hupelekea kupotea kwa mikoko na kuathiri ukuaji wa uchumi wa bluu.

Naye, Kamishna wa Uhifadhi, Wakala wa Huduma za Misitu za Misitu Tanzania, Prof Dos Santos Silayo amesema wananchi wanatakiwa wawe na mifumo endelevu ya kupata kipato itakayowawezesha kukidhi mahitaji yao bila kukata mikoko.

“Mifumo hii itawawezesha wananchi kuvuna hewa ya ukaa na kujipatia fedha bila kuathiri mikoko kwa mfano kufanya shughuli za ufugaji nyuki na utalii” amefafanua Prof. Silayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uvuvi, Wizara ya Uchumi wa Bluu Zanzibar, Dkt. Salumu Hemedi amesema kuna uhusiano mkubwa wa uchumi wa bluu na biashara ya hewa ya ukaa inayofanyika katika mataifa mengi duniani ambayo yana viwanda yanatumia hewa ya ukaa katika nchi ambazo zina misitu ambazo zinalipwa ili kutunza misitu.

Warsha hiyo, imehudhuriwa wa Maafisa kutoka Serikali ya Tanzania na Kenya, Wawakilishi wa Sekta Binafsi, Wadau wa Uhifadhiwa Mifumo Ikolojia ya Bluu pamoja na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania.

Mkakati uendelezaji sekta ya Sheria waandaliwa
Shambulio la msafara lauwa askari 11