Miley Cyrus ameendelea kukimbizwa na mzimu wa ukosoaji alioutoa mwaka 2017 dhidi ya muziki wa kufokafoka aka hip-hop na ameamua kuwapigia magoti mashabiki.

Katika mahojiano yake na Billboard mwaka 2017, mwimbaji huyo alidai kuwa amejitenga na hip-hop kwa sababu umekuwa muziki wa kusifia magari, pombe na ngono.

“Siku hizi sisikilizi tena hip hop,” alisema Miley alipokuwa anatangaza albam yake ya ‘Young Now’. Aliongeza, “hicho ndicho kilichonisukuma mbali kidogo na hip-hop. Ilikuwa imepita kiasi, kila ukiwasikia wanasifu ‘Lamborghini, mara nimepata Rolex, nina demu wangu mkali’… mimi sio wa hivyo hata kidogo.”

Mashabiki wa muziki huo walimvaa Cyrus, hususan kwa kuzingatia kuwa albam yake ya mwaka 2013 iliyokuwa inaitwa ‘Bangerz’ aliwashirikisha wasanii wa hip-hop na baadhi ya nyimbo zake pia zilikuwa na maneno kama aliyoeleza kuyakosoa.

Hivi karibuni, shabiki mmoja ambaye ni mtumiaji wa YouTube, Kenya Wilson alitonesha kidonda na kurudisha kumbukumbu za mkasa ule ambapo alimueleza Miley Cyrus kuwa yeye bado ni tatizo kwake kwa aliyoyasema kuhusu hip-hop.

Kutokana na mashambulizi mapya ya mashabiki, Miley aliamua kuomba radha kwa maelezo marefu lakini kikubwa alisema ni kitu ambacho kimekuwa kikimuumiza pia kwa muda mrefu.

“Asante kwa kunipa nafasi ya kuzungumza tena. Kuwa kimya sio tabia yangu hata kidogo. Ninafahamu njia zangu za kuufikia umma na siku zote ninazitumia kwa namna bora zaidi,” alisema.

“Ninaomba kusema naomba radhi, ni dhahiri kuwa matamshi yangu ya kujitenga na hip-hop hayakuwa mazuri na sikufikiria vizuri zaidi kwa uwezo wa kuchimba ndani na nje kuona madhara yake. Kwa ufupi naomba kusema nilizingua sana, ninapaswa kutumia sauti yangu kuponya, kuunganisha na kusimamia kilicho na haki, nisameheni,” aliongeza.

Hata hivyo, baada Bangerz aliachia Miley Cyrus & Her Dead Petz ambayo haikuhusisha kabisa hip-hop.

Tiketi zinawahusu waliotemwa Taifa Stars
WHO yachukua hatua za dharula kuhusu Ebola nchini Uganda

Comments

comments