Serikali nchini kupitia Wizara ya Afya, imetoa zaidi ya Shilingi milioni 200 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya Afya katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa Bombo,Tanga.

Mganga Mkuu wa Mkoa Mkoa wa Tanga, Dkt. Jonathan Budenu ameyabainisha hayo wakati akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa huduma na utekelezaji wa miradi ya afya katika mkoa huo chini ya ufadhili wa Shirika la Fedha Duniani (IMF).

Amesema, pamoja na maboresho mbalimbali pia fedha hizo zimetumika katika kukarabati jengo la wagonjwa mahututi (ICU), ambalo tayari limeanza kutoa huduma kwa wagonjwa sambamba na kukamilishwa kwa ukarabati wa jengo la Huduma za Dharura.

“Ukarabati wa majengo hayo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa ukilinganisha na hali ilivyokuwa hapo awali ambapo wagonjwa walilazimika kusubiri kukamilika shughuli nyingine ambazo zilikuwa zikitegemea chumba hicho kabla ya wao kupatiwa huduma,” amesema Dkt. Budenu.

Aidha, ameongeza kuwa matibabu katika Jengo la Huduma za Dharura yanatarajiwa kuanza katikati ya mwezi Julai mwaka huu, kitu ambacho kitasaidia kutoa usumbufu uliokuwepo awali wa kukosekana kwa jengo hilo.

Awali, wakati akizungumzia hali ya utoaji huduma za Afya katika Mkoa wa Tanga, Dkt. Budenu ameishukuru Serikali kwa kujenga Hospitali tano mpya ambapo tayari Hospitali tatu za Muheza, Korogwe na ile ya jijini Tanga zimeshaanza kutoa Huduma, huku Hospitali ya Handeni ikitarajia kuanza kutoa huduma mwishoni mwa mwezi Julai na Kilindi kuanza mwezi Agosti 2022.

Serikali kupitia Wizara ya Afya tayari imejenga vituo vya Afya 17 Mkoani Tanga, ambapo vituo saba kati ya hivyo vinatarajiwa kuanza kutoa huduma mwishoni mwa mwezi Julai 2022 huku shukrani zikitolewa kwa Serikali kutokana na kusaidia kukabiliana na changamoto ya watumishi kupitia ajira mpya zilizotolewa na Serikali kwa watumishi wapya wapatao 200 kupelekwa mkoani Tanga.

Try Again amaliza mikwaruzano Simba SC
Wanahabari wajiuliza marekebisho vifungu vya sheria