Mshambuliaji wa pembeni wa klabu ya Liverpool, James Milner amesema anaamini matokeo ya sare ya bila kufungana dhidi ya Tottenham Hotspurs, yameonyesha dhamira ya kweli ya meneja mpya wa klabu hiyo Jurgen Klopp.

Milner ambaye alikua sehemu ya kikosi cha Liverpool mwishoni mwa juma lililopita, amesema kulikua na hali tofauti kikosini kwao, kutokana na umakini wa meneja huyo kutoka nchini Ujerumani, hivyo anaamini kuna jambo kubwa lipo njiani linakuja.

Amesema katika mchezo dhidi ya Spurs, kila mchezaji alikua anajihisi ni mpya, na alipambana kwa nguvu zake zote, na ilionyesha dhahir nini walichokua wakikihitaji katika mpambano huo ambao ulichezwa kwenye uwanja wa White Hart Lane.

Hata hivyo Milner amewataka mashabiki wa soka kutoichukulia vibaya kauli yake ya kumsifia Klopp, kwa kuona labda hakupendezwa na utawala wa meneja aliyetimuliwa huko Anfield majuma mawili yaliyopita Brendan Rodgers.

Amesema Rodgers, bado ana ubora wa kipekee na daima ataendelea kumshukuru kwa mazuri aliyoyafanya klabuni hapo, lakini akasisitiza kwamba kila meneja aliyepita Liverpool ana ubora wake.

Klopp atakuwa na mtihani mwingine mwishoni mwa juma lijalo, pale kikosi chake kitakaporejea Anfield kuendelea na michezo ya ligi ya nchini England kwa kupambana na Southampton.

Ajira Ya Tim Sherwood Yaning'inia
Kamati Ya Taifa Stars Yatambulishwa Rasmi