Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza viongozi na wazazi wilayani Siha mkoani Kilimanjaro washirikiane kuhakikisha watu wote waliowapa mimba wanafunzi wanasakwa na kufikishwa kwenye vyombo vya dola.

Majaliwa amesema katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Desemba mwaka jana jumla ya wanafunzi wa kike 57 walikatishwa masomo baada ya kupata mimba na hadi sasa kesi zilizofunguliwa ni sita tu.

“Jambo hili halipendezi, kesi sita tu ndio zimefikishwa mahakamani. Hakikisheni wahusika wote waliowapa mimba wanafunzi wanatafutwa popote walipo, wakamatwe na wachukuliwe hatua kali za kisheria.”

Majaliwa amesema hayo Februari 24, 2019 alipokuwa akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Isanja, Sanya Juu wilayani Siha wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Kilimanjaro.

Amesema Serikali imeweka sheria kali ya kumlinda mtoto wa kike lengo ni kumuwezesha amalize masomo yake ili aweze kujikwamua kiuchumi na aondokane na utegemezi, hivyo ni marufuku kuwakatisha masomo.

Watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii na Serikali itatoa adhabu kali ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu atakayekatisha elimu ya mtoto wa kike iwe kwa kumuoa, kumpa ujauzo na hata ukikutwa naye nyumbani kwako, katika nyumba ya wageni.

“Tukikukuta na binti wa shule katika kona isiyoeleweka tunakukamata na kukuchukulia hatua za kisheria. Ole wenu vijana, mkibainika mmewapa mimba mabinti wanaosoma, adhabu yake ni miaka 30 jela, sasa tafakari kabla ya kutenda.”

Amesema kwa wazazi au walezi watakaowaozesha watoto wa kike ambao bado ni wanafunzi na kwa upande wa wazazi watakaomsindikiza mtoto kwenda kuoa mwanafunzi wote watachukuliwa hatua za kisheria.

“Kuna taarifa nimezipata kuwa baada ya watoto kupewa mimba wazazi au walezi mnamalizana na wahusika kwa kupeana ng’ombe. Sasa tukikukamata unamalizana na mtu aliyempa mimba mwanafunzi na wewe tunakufunga.”

Mahakama yatoa uamuzi hati ya kumkamata Lissu, yawaonya wadhamini
Sarri afunguka baada ya golikipa kugoma kutoka na kufungwa