Utata umeibuka kufuatia taarifa zilizotolewa jana jumanne (Machi 31) katika mitandao ya kijamii kuhusu uongozi wa klabu ya Alliance FC, kuachana na kocha Fred Felix Minziro.

Minziro amekua kocha mkuu wa Alliance FC kwa miezi kadhaa, baada ya kuachana na Singida United ambapo alishindwa kuendana na falsafa za klabu hiyo ambayo ina kila dalili za kushuka daraja.

Saa chache baada ya kutoka kwa taarifa za kuondoka kwa Minziro, ilielezwa kuwa kocha huyo mzawa amejiunga na Pamba FC ya jijini Mwanza inayoshiriki ligi daraja la kwanza.

Kutokana na taarifa hizo, Mwenyekiti wa Mashindano wa Alliance FC Yusuf Budodi amekanusha kwa kusema hakuta ukweli wowote kuhsu uongozi wa klabu hiyo kumuondoa Minziro na bado wanatambua ni muajiriwa halali.

“Sio kweli. Ni taarifa ambayo hata mimi ilinistua, nilikuwa kwenye mazingira ya sintofaham kwa sababu nilikuwa kwenye mapumziko ya wiki moja lakini nilipigiwa simu na nikatoa ufafanuzi kwamba Minziro bado ni kocha wa Alliance mpaka sasa”-Yusuf Budodi, Mwenyekiti wa Mashindano.

“Kuna mazingira ambayo yamejitokeza kwenye kituo, sisi tuna timu nyingi kwa hiyo kuna makocha wameongezeka halafu tayari kuna kocha ambaye yupo, watu wanajiuliza huyu anaendelea na majukumu au anaondokewa?

“Tunachofahamu Minziro bado kocha wa Alliance na nilizungumzanae kwa simu nikamwambia kuhusu hizi taarifa, akaniambia hata yeye amepigiwa sana simu. Bado yupo Alliance na anamkataba, hizi ni tetesi tu.”

Hata hivyo kwa upande wa kocha Minziro amesema: “Sina habari hizo, sijui. Sijapata habari yoyote mimi, mtafute mwenye timu umuulize labda anauhakika kama kweli au si kweli. Bado ninamkatabanao wa miezi sita kwa hiyo siwezi kuzungumza chochote kwa hivi sasa”-Felix Minziro-Kocha.

“Hata zikiwa habari za kweli mimi sijapata barua, siwezi kuongea chochote.”

Kwa upande wa Pamba FC kupitia kwa kaimu Katibu wa Pamba SC, Johnson James amesema: “Tunachoweza kusema kama klabu, kocha Minziro hatukuachananae vibaya alikuwa miongoni mwa makocha ambao tumefanyanao kazi vizuri na aliifundisha timu yetu kwa muda mfupi lakini ilibadilika sana.”

“Taarifa za kurejea kwake zinaweza kuwepo kwa sababu kuna kamati inashughulika na hilo suala. Kama litakuwepo taarifa italetwa kwangu na kamati ya ufundi. Ikitokea akarudi itakuwa ni jambo jema na sisi tutashukuru.”

Endapo Minziro atakuwa ameachana na Alliance FC, atakuwa kocha wa nne (4) kuachana na timu hiyo ndani ya msimu mmoja wa ligi kuu, akitanmguliwa na Athumani Bilali ‘Billo’, Malale Hamsini na Habibu Kondo.

Alliance FC ipo kwenye hatari ya kushuka daraja, ipo nafasi ya 18 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 29 baada ya kucheza mechi 29.

Benki ya Dunia yaridhia kuikopesha Tanzania $500 milioni za elimu
Uingereza: mvulana wa miaka 13 afariki dunia kwa Covid 19