Mataifa ya Misri na Ivory Coast yamefuzu kushiriki michuano ya Olimpiki 2020, itakayofanyika Tokyo, Japan, baada ya timu zao za taifa chini ya umri wa miaka 23 kutinga hatua ya fainali.

Mataifa hayo yametinga hatua ya fainali ya michuano ya Afrika chini ya umri wa miaka 23, inayoendelea nchini Misri, kwa kuzitupa nje Afrika kusini na Ghana.

Wenyeji Misri waliibanjua Afrika kusini mabao matatu kwa sifuri, kwenye mchezo wa nusu fainali, huku Ivory Coast wakiichabanga Ghana kwa changamoto ya mikwaju ya penati.

Misri waliokua wanacheza mbele ya mashabiki wao, walipata bao la kwanza kwa njia ya mkwaju wa penati kupitia kwa Ramadan Sobhy dakika ya 59, huku Abdel Rahman Magdy akifunga mabao mawili na kukamilisha ushindi wa mabao matatu kwa sifuri, uliowavusha hadi hatua ya fainali.

Hata hivyo mshiriki watatu kutoka Afrika kwenye michuano ya Olimipiki 2020, anatarajiwa kufahamika baada ya mchezo wa kumsaka mshindi wa tatu na wanne, utakaochezwa kesho Ijumaa, kati ya Ghana na Afrika kusini.

Michauno ya Olimpiki 2020 imepangwa kuanza kuunguruma mjini Tokyo, Japan kuanzia Julai 24 hadi Agosti 09, huku michuano ya soka ikipangwa kuanza kutimua vumbu kuanzia Julai 22 hadi Agosti 08.

Katika michuano hiyo upande wa wanaume timu kumi na sita zitashiriki, huku wanawake wakitarajiwa kuwa na timu kumi na mbili, kutoka kwenye mabara yote.

Viwanja saba vitatumika kushuhudia miamba upande wa wanaume na wanawake ikimenyana ambavyo ni, National Stadium (Shinjuku,Tokyo), Tokyo Stadium (Chofu, Tokyo), Saitama Stadium (Saitama), Int. Stadium Yokohama (Yokohama, Kanagawa), Ibaraki Kashima Stadium (Kashima, Ibaraki), Miyagi Stadium (Rifu, Miyagi) na Sapporo Dome (Sapporo, Hokkaido).

Ummy azitaka Halmashauri kutekeleza miradi inayogusa jamii
Video: JPM hakuna bei elekezi ya mahindi, Mtoto miaka 9 kutunukiwa degree mwezi ujao