Maneno ya kukatisha tamaa ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya Viongozi wa Serikali juu ya vipengele kandamizi katika tasnia ya habari zimeonekana kuwa mwiba katika muhimili huo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wanahabari hao wamesema ufanyaji wa Kari usio na uhuru au wenye kuminya mirija ya utendaji ni hatari kwa mustakabali wa maendeleo ya Habari.

Malalamiko hayo, yanafuatia mapendekezo ya Serikali katika kuboresha vifungu mbalimbali ambavyo ni tata ikiwemo kile cha kutaka magazeti kupata usajili wa kila mwaka badala ya ule wa awali wa usajili wa kudumu.

Kauli nyingine ni ile iliyotolewa na aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,Innocent Bashungwa juu ya nia ya Serikali kuendelea na taratibu za

kuanzisha Bodi ya Ithibati itayokuwa na jukumu la kutoa ithibati navitambulisho kwa wanahabari wenye sifa.

Wanasema, endapo bodi hiyo ya ithibati itaanzishwa itakosa uhuru wa kufanya mamuzi hasa pale malalamiko yatakapokuwa yanaihusu Serikali.

“Yapo mambo yanatafakarisha, ujue zama zimebadilika na tunapaswa kuendana nazo maana Dunia ya sasa inahitaji uwazi na ukweli sasa kwa mtindo huu endapo utafanikiwa uhuru wa Habari utakuwa umefungwa minyororo,” amesema Mwanahabari Felix Daniel.

Mapendekezo hayo ya baadhi ya wanahabari ambayo mengi yamekuwa yakishabihiana kutokana na ukweli kuwa tasnia hii inahitaji kuwa huru yanasema ili kutenda haki kwa vyombo vyote vya habari nchini, basi Bodi hiyo inabidi iundwe na kusimamiwa na wanataaluma husika.

Wanasema, “Uandishi wa kusifia au ulioegemea eneo moja pekee una akisi kutokuwa na uhuru halisi kwani itashindikana kuhoji pale mambo yanapoenda kombo na hivyo kuondoa maana halisi ya uhuru wa vyombo vya Habari.”

“Kushindwa kuhoji mambo kutatokana na woga wa kuchukuliwa hatua au kuwajibishwa na kupewa adhabu kwani endapo sheria hizo zitafanyiwa mabadiliko zitaipoka mamlaka ya muhimili wa Habari na kukosa mtetezi,” amesema mwandishi Alfred Kilatu.

Aidha, wanaarifu kuwa, tasnia mbalimbali nchini zimeunda na kusimamia bodi zao bila kuingiliwa na serikali, hali inayotoa mshangazo kwa Serikali kupendekeza kuunda bodi hiyo badala ya kuwaacha wanahabari kuunda na kujisimamia.

Hata hivyo, wapo baadhi ya watu wenye mapenzi Emma na tasnia ya habari, akiwemo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Eliezer Feleshi  ambaye alisema ni vizuri Bodi ya Ithibati ya Habari ikaundwa na kusimamiwa na wanahabari wenyewe.

Jaji Feleshi alitoa maoni hayo Mei 13, 2022 wakati alipokutana na wadau wa habari wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Julai 14, 2022 
Serikali yatoa tamko ugonjwa mpya Lindi