Mkazi wa wilaya ya Babati mkoani Manyara aliyejitambulisha hivi karibuni mbele ya Rais John Magufuli kwa jina la Mwanaidi na kwamba ni mjane aliyedhulumiwa mali za mumewe na mke mdogo, amefutwa machozi.

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Crispin Meela ametekeleza agizo la Rais Magufuli la kumtaka ahakikishe mjane huyo anapata haki yake ikiwa ni pamoja na kukabidhiwa nyumba na shamba alilodai amepokonywa na mke mdogo baada ya mumewe kufariki.

Juzi, Meela amemkabidhi mjane huyo nyumba na shamba la ekari 2.5 na kueleza kuwa kama mke ndogo anaona hakuridhishwa na uamuzi uliofanywa ana haki ya kukata rufaa mahakamani.

Mke mdogo aliyejitambusha kama Asia Musa ameendelea kudai kutotendewa haki kwani nyumba hiyo aliyokabidhiwa mke mkubwa aliijenga yeye na mumewe. Hata hivyo, Mwanaidi naye ameendelea kusisitiza kuwa mke mdogo aliikuta nyumba hiyo akiwa ameijenga yeye na mumewe.

Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wananchi kuwa makini na kufuatilia kwa ukaribu sheria ya miradhi na ardhi ili kuondoa migogoro.

“Migogoro ya mirathi imeendelea kukithiri katika maeneo mengi nchini kutokana na watu kutofuata sheria za mirathi na wengine wakitaka kunufaika na mali zinazoachwa na marehemu,” alisema Meela.

 

Marekani wafanikiwa kupandikiza Uume unaofanya kazi
Makamu wa Rais awasha moto, awapa ‘dedilaini’ wakuu wa Mikoa na Wilaya