Awena Sinani Masoud, aliyekuwa mke wa Hayati Maalim Seif Shariff Hamad, amezungumza juu ya masuala ya kisiasa na kijamii katika wasaa wa mahojiano maalumu na Dar24 na kueleza mengi kwa undani juu ya maisha ya aliyekuwa mume wake.

Akifahamika zaidi kama Aunt awena, Mjane huyo wa Hayati Maalim Seif Sharif Hamad amesema mpaka umauti unamfika, Mumewe aliipenda Serikali na Mapinduzi ya Zanzibar na alifanya jitihada kubwa kuhakikisha amani inatawala katika visiwa hivyo.

Aunt Awena amesema kuwa Maalim alikuwa na mahusiano mazuri na viongozi wote wa kitaifa ikiwa ni pamoja na kumsifia Rais wa Sasa wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuwa ni mtu anaependa amani na asietaka makuu.

Amesema kuwa mahusiano kati ya Hayati John Pombe Magufuli na Maalim Seif Sharif hamadi hayakua na mtafaruku kwani wawili hao walikua wakikutana wanazungumza vizuri na walikua wanawasiliana vizuri kama viongozi wa Tanzania.

“Siwezi zungumza undani wao wala sijui wamepanga nini lakini najua walikua wanazungumza vizuri kama viongozi wa Tanzania, wanashauriana tena nyuma ya pazia kila mtu anajua mwenyewe, najua mie kwa mbele ya macho yetu wanazungumza vizuri,” alisema Awena.

Aunt Awena anasema kuwa familia iliamua kuweka wazi sababu za kifo cha Hayati Maalim Seif kwa sababu walitaka kuwanusuru wananchi juu ya ugonjwa wa UVIKO 19 kwa kuwataka wajikinge na wachukue tahadhari.

“Ni kwa sababu tulitaka jamii ijue kuwa hili swala lipo na huwezi kuficha maradhi, kwa sababu mficha maradhi mauti yatamfichua, huwezi kufiicha maradhi wakati unayo, utangazie umma, wajue kwamba kuna maradhi na watu wachukue tahadhari. Kwa sababu ukisema hakuna maradhi ni kuwaachia watu free, watu wanakula, wanatembea, wanafanya mashughuli hawana wasiwasi. lakini ukitangaza kila mtu atachukua tahadhari. Hivyo tulitangaza ili kupunguza athari na naamini hata maambukizi yalipungua.” Alisema Awena.

Aidha Aunt Awena anaongeza kuwa baada ya Maalim Seif kuingia katika uongozi alishirikiana vizuri na Chama Tawala cha CCM, na malengo yake ya muda mrefu ilikua ni kuweka watu pamoja, kushirikiana, na kupeleka mbele taifa letu.

“Nahisi baada ya kuingia kwenye uongozi hata kama kna mtu alikua na chuki nae, zilipungua kwa kiasi fulani kwa sababu yeye aliamua kutembeza ziara Unguja na Pemba ili kuwaweka watu sawa na kuleta ushirikiano,”

Aidha kuhusu ukaribu wa Hayati Maalim Seif na Makamu wa Rais wa sasa huko visiwani Zanzibar ni kweli kulikua na mahusiano ya karibu zaidi kwa sababu walishirikiana sana na mambo mengi walipeana miongozo ya uongozi na kulikua na usiri mkubwa kati ya ukaribu wao na ni kweli alimuandaa kuwa kiongozi atakayemrithi.

Aunt Awena alisema katika enzi za uhai wake Maalim alikua ni baba mzuri wa familia na alijua kutenganisha familia na siasa, na kutokana na hili aliweza kutenga muda kwa ajili ya familia na kufanya majukumu yake yote kama baba na hakuwa na tabia ya kuleta maswala ya siasa nyumbani.

Katika kutoa ushauri kwa wanasiasa Awena amewataka wanasiasa wote kuacha chuki ambazo zinazosababisha watu kutoshirikiana katika masuala ya kijamii kama mazishi na shughuli za furaha.

Hayati Maalim Seif Sheriff Hamad alifariki dunia akiwa Mwanasiasa mkongwe (76) na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Februari 17, 2021, katika Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa takribani wiki mbili kutokana na Ugonjwa wa UVIKO 19

Mahojiano ya Mjane wa Maalim Seif na Stanslaus Lambat

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Januari 18, 2022
Simba SC yaacha alama tatu Mbeya