Tamko la Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kuhusu mapungufu kwenye sekta ya elimu nchini limemuibua Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye amedai hiyo ilikuwa ajenda yake kuu.

Hivi karibuni, Mkapa alieleza kutoridhishwa na hali ya elimu nchini akidai kuwa imekuwa janga ambalo linahitaji mhahalo wa wazi ili kulitafutia ufumbuzi.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, Lowassa ameeleza kufurahishwa na kauli ya Mkapa akidai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshindwa kuisimamia ipasavyo sera hiyo.

Amesema kuwa suala la elimu bure kuanzia shule ya msingi ilikuwa ajenda yake akiwa ndani ya CCM na hata alipohamia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kwamba iko kwenye ilani ya uchaguzi ya chama hicho kikuu cha upinzani.

“Nachelea kusema kuwa hii sio ajenda ya Serikali ya CCM, hawataweza kulisimamia kwa sababu wanataka kuendelea kutawala na hawataki kuwa na taifa lililoelimika vizuri, linaloweza kuhoji,” amesema.

CCM imejibu kauli hiyo ya Lowassa kupitia Katibu wake wa Itikadi na Uenezi upande wa Zanzibar, Catherine Peter. Amesema kuwa sio kweli kwamba CCM imeshindwa kutekeleza sera hiyo ambayo amekiri kuwa ililetwa na Lowassa akiwa CCM kama mwanachama na baadaye kuihamishia upinzani.

“CCM inapenda kuongoza watu wenye elimu na ndiyo maana inatoa elimu bure ili kuwapa watoto fursa ya kusoma na kuelimika zaidi. Hivyo, sio kweli kwamba CCM inataka kuongoza wajinga,” Catherine anakaririwa na Mwananchi.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo amesema kuwa wameyapokea maoni ya Mkapa na kwamba watayafanyia kazi kwa kujumuisha wadau wengine.

UNESCO: Kuna upungufu mkubwa wa maji safi duniani
Trump ataka wauza 'unga' wahukumiwe kifo