Wadau wa sekta ya elimu wametakiwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) katika kuboresha sekta hiyo ili iweze kuendana na uhitaji uliopo.

Kauli hiyo imetolewa mkoani Dar es salaam na Katibu Mkuu wa wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo, wakati wa hafla ya kusaini makubaliano kati ya TET na Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) ya uandishi wa vitabu 32 vya kiada vya masomo ya ufundi.

Amesema Serikali imekuwa ikijitahidi kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu nchini, lakini wadau wa sekta hiyo na TET wanatakiwa kuendelea kuboresha mifumo ya elimu hasa kwa kuangalia masuala ya mitaala na mihutasari.

“Kulikuwa na malalamiko ya watu wa elimu juu ya mitaala na mihtasari ya elimu ya ufundi kutokuwepo, nadhani kwa hili Taasisi ya elimu mmefanya vizuri na utasaidia Wananchi wetu katika kujipatia elimu ya ufundi itakayopelekea kujiajiri au kuajiriwa.” ameeleza Dkt Akwilapo.

Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt Aneth Komba amesema utiaji saini wa makubaliano hayo kati ya TET na DIT ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali katika kuwezesha ukuaji wa sekta ya elimu nchini.

“Serikali ya awamu ya sita imekuwa ikisisitiza namna ya Wadau wote kushirikiana katika kuboresha mfumo wa elimu, na sisi kama Watendaji wa Serikali tutaendelea kulisimamia hili ili kufikia lengo lililowekwa katika kuleta ufasi katika sekta ya elimu.” amesema Dkt Komba

Pia ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuiamini tasisi hiyo kwa kuirejeshea majukumu ya uandaaji mitaala jambo ambalo miaka ya nyuma lilisitishwa.

Kwa upande wake Mkuu wa DIT Profesa Preksedis Ndomba amesema ushirikiano wao na TET utasaidia kuandaa mitaala na mihtasari itakayokuwa na uhitaji sahihi.

Almasi ya tatu kwa ukubwa yapatikana Botswana
Festo Sanga amshukuru Rais Samia