Kufuatia taarifa zilizosambaa mitandaoni kuwa huenda aliyekuwa bingwa wa masumbwi nchini, Francis Cheka alikuwa  mmoja kati ya waathirika wa ajali ya moto katika eneo la Msamvu mjini Morogoro iliyotokea baada ya roli la mafuta kulipuka, mkewe amejitokeza na kukanusha.

Mke wa mwanamasumbwi huyo anayefahamika kama Toshi Azenga ameeleza kushangazwa na taarifa hizo, akiweka wazi kuwa mumewe yuko salama na anaendelea na shughuli zake.

Azenga amekaririwa na gazeti la Mwanaspoti akidai kuwa mumewe huyo aliyekuwa anaishi Morogoro hivi sasa amehamishia makazi yake nchini Msumbiji pamoja na mkoani Mtwara. Taarifa hizo pia ziliwahi kutolewa na bondia huyo katika mahojiano aliyofanya hivi karibuni akieleza kuwa anajihusisha na kazi ya kukusanya makopo pamoja na kupromoti michezo ya masumbwi.

Cheka ni mmoja kati ya wanamasumbwi waliosaidia kukuza mchezo huo nchini, akipigana ndani na nje ya nchi. Aliwahi kuwa mbabe wa kwanza kuwatoa kwenye reli ya ubabe familia ya akina Rashid Matumla. Hata hivyo, alipoteza pambano lake la mwisho dhidi ya Dulla Mbabe baada ya kupigwa kwa KO na kutangaza kutundika ‘gloves’.

Taarifa zilizomhusisha bondia huyo na ajali ya moto zilidai kuwa alionekana kwenye eneo hilo wakati watu wanachota mafuta ya petroli kutoka kwenye roli lililopinduka lakini tangu wakati huo hakuonekana tena na simu zake hazikuwa zinapatikana.

Tukio hilo lilisababisha vifo vya watu 76 na baadhi ya miili ilishindwa kutambulika kutokana na kuharibika vibaya na ilizikwa na Serikali katika makaburi ya Kola Hill mjini Morogoro.

 

 

 

Waziri Mkuu azindua Mwongozo wa Uwekezaji mkoani Kagera
Mhadhiri NIT aburuzwa mahakamani kwa rushwa ya ngono