Sakata la ununuzi wa mabehewa kwa ajili ya Shirika la Reli Tanzania (TRL) yanayodaiwa kuwa mabovu liliibuka jana Bungeni na kumuinua Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye alikuwa Waziri wa Uchukuzi katika serikali ya awamu ya nne.

Waziri Mwakyembe alikanusha madai yaliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Jesca Kishoa kuwa ununuzi huo wa mabehewa mabovu yaliisababishia sherikali hasara ya shilingi bilioni 238, huku akitaka ripoti ya ukaguzi wa ununuzi huo iwasilishwe bungeni.

Akitumia kanuni ya 63 (3) kuomba kutoa taarifa, Mwakyembe alikanusha kiwango cha fedha kilichotajwa na mbunge huyo wa viti maalum ambaye ni mke wa aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila.

“Mbunge aliyesimama kabla, aliyejitambulisha kama mke wa Kafulila, ameeleza kwamba serikali ilitumia zaidi ya shilingi bilioni 238 na kuleta hasara kwa kununua mabehewa mabovu. Mheshimiwa Mwenyekiti nataka kukuthibitishia kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kwa kununua mabehewa 274 haijawahi kutumia zaidi ya shilingi bilioni 60,” alisema Mwakyembe.

Waziri huyo alienda mbali na kueleza kuwa endapo mbunge huyo atawasilisha uthibitisho wa kiwango hicho cha fedha kutumika kununua mabehewa hayo, atajiuzulu nafasi yake ya ubunge.

“Mimi naomba athibitishe hiyo shilingi bilioni 238. Na nitashukuru sana kama akileta hapa. Na akileta hiyo, mimi nitajiudhuru hata ubunge,” alisema Mwakyembe.

Baada ya kauli hiyo ya Mwakyembe, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee naye alisimama na kueleza kuwa Waziri huyo hakutumia kifungu sahihi kutoa taarifa kwa kuwa alipaswa kutumia kifungu cha 63 (4) kutoa ushahidi wa kukanusha kwake kwanza.

Naye Kishoa aliendelea kusisitiza kuwa Serikali inapaswa kuwasilisha bungeni hapo ripoti ya ukaguzi wa manunuzi ya mabehewa hayo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge, Dk. Mary Mwanjelwa alitoa siku tatu kwa mbunge huyo wa viti maalum kuwasilisha ushahidi kuhusu madai yake.

Tanzia: Diwani wa CUF AUAWA KWA MAPANGA
Thamani Ya Usajili Yapanda Kwa Bilioni 1