Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu jana alilala rumande baada ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi kwa zaidi ya saa tatu katika kituo kikuu jijini Dar es Salaam, kwa tuhuma za kutoa maneno yenye uchochezi katika mkutano wake wa hadhara alioufanya jimboni kwake hivi karibuni.

Lissu ambaye alisafirishwa umbali wa Kilomita 687 kutoka Singida, alisababisha ulinzi mkali kuimarishwa kituoni hapo huku viongozi wa ngazi ya juu wa Chadema pamoja Waziri Mkuu wa Zamani, Edward Lowassa kuwasili katika kituo hicho .

Mbali na viongozi hao, Mkewe, Alicia Magabe alifika kituoni hapo na kuzungumza na mumewe ambaye baadae aliwaeleza waandishi wa habari kilichojili.

Alicia aliwaeleza waandishi wa habari kuwa baada ya kuonana na Lissu, mwanasiasa huyo alizungumza naye na alimlilia kuwa ana njaa, ndipo alipomtafutia chakula kabla ya kuanza kuhojiwa na Polisi.

Mke wa Mbunge huyo wa Singida Mashariki alisisitiza kuwamumewe hatarudi nyuma katika kupigania kile anachokiamini, na kwamba endapo atamuona yuko kimya kutokana na hayo atajua sio ‘Tundu Lissu anayemfahamu’.

Katika hatua nyingine, Alicia elieleza kuwa juzi watu wanne ambao anaamini walikuwa askari polisi walifika nyumbani kwake wakiwa na gari aina ya Noah nyeusi na walikuwa wakimtafuta mumewe.

Alisema watu hao hawakuwakuta yeye na Lissu na walimuulizia dada wa kazi ambaye aliwaeleza kuwa hawapo.

“Baadae walivyomaliza walionekana wakiwasiliana kwa simu. Msichana wangu wa kazi aliwasikiwa wakisema kwenye simu ‘hayupo nyumbani kwake, tumemkosa’, kisha wakaondoka,” alisema Alicia.

Lissu anatarajiwa kufikishwa Mahakamani leo kujibu tuhuma zinazomkabili.

Fernando Llorente Kutimkia Liberty Stadium
Kiwanda Cha Nguo Nida Textile Chatozwa Faini Milioni 30 Kwa Uchafuzi Wa Mazingira