Mke wa mwanamuziki Proffesor Jay ameendelea kudhihirisha kuguswa kwa na mapenzi ya wadau mbalimbali walioungana na familia ya mwanamuziki huyo katika kuhakikisha wanashiriki kwa hali na mali kuipambania afya ya nyota huyo wa muziki aliyekuwa akisubuliwa na maradhi yaliyompelekea kulazwa hospital kwa kipindi cha takriban siku 127.

Mke huyo wa Prof. Jay ameutumia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram kushukuru kwa kila aliyeguswa na kushiriki katika kuipambania afya ya mumewe.

“Kwa niaba ya Familia ya Joseph Leonard Haule (Prof. Jay) Tunamshukuru Mungu muweza wa yote kwa kuendelea kuiimarisha Afya ya Prof. Jay siku hadi siku mpaka leo.

Kwa upekee kabisa tunamshukuru Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa tamko la Serikali yake kugharamia gharama zote za Matibabu ya Joseph Haule (professor Jay ) tunashukuru sana sana na sisi Kama Familia hatuna cha kumlipa bali tunamuombea Kwa Mwenyezi Mungu azidi kumbariki Rais wetu pamoja na Serikali yake .

Tunamshukuru Rais mstaafu wa awamu ya nne Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, tunaushukuru uongozi, Madaktari pamoja na wauguzi wote wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Lugalo na Kitengule.

Tunalishukuru Bunge la Tanzania chini ya Spika Dr. Tulia Ackson, viongozi wakuu Chadema na CCM pamoja na wanachama wake wote, kuweka itikadi ya vyama pembeni na kushughulikia afya ya Prof. Jay mpaka hii leo.

Tunashukuru Wizara mbali mbali haswa Wizara ya Afya (Ummy Mwalimu), Kwa jitihada mlizozionyesha Kwa kuhakikisha Joseph anapata matibabu ya uhakika, Wizara ya Sanaa (Mohamed Mchengerwa) Kwa kuendelea kumtambua Kwa mambo mbali mbali yaliyo kuwa yakiendelea pamoja na kuwa amelala kitandani .

Tunawashukuru Viongozi mbali mbali wa Dini zote Kwa kujitolea kumuombea sana Joseph bila kuchoka.

Vilabu vya Soka kama Simba, Yanga na vilabu vingine. Tunavishukuru pia Vyombo vyote vya habari (TV, Radio na Online media), Bila kuwasahau wananchi wote wa Tanzania ndani na nje ya Tanzania ambao wamekuwa wakimuombea na kumtakia kila la kheri aweze kurudi Sawa.

Mwisho Tunawashukuru Ndugu, Jamaa, Marafiki na Mashabiki wote wa Profesa Jay kwa kumuombea Jay kila siku bila kuchoka. Mungu awabariki sana hatuna cha kuwalipa” unasomeka ujumbe wa mke wa Prof Jay.

Hali ya afya ya mwanamuziki Prof Jay kwa sasa inaendelea vizuri huku afya yake ikiendelea kuimarika ambapo ameruhusiwa kurudi nyumbani anakoendelea na hatua za kuiimarisha zaidi afya yake.

Habari kuu kwenye magazeti ya leo Juni 15, 2022 
Viwanja vitano kuwekwa Nyasi Bandia