Mke wa msanii Roma Mkatoliki amefunguka juu ya wimbo mpya wa mume wake  uliobatizwa jina la ‘Zimbabwe’ kuwa aliupa baraka zote  kwani ni mmoja kati ya watu wanaozipitisha kazi za rapa huyo.

Alisema kuwa baada ya kuusikiliza wimbo huo hakutaka neno lolote lipunguzwe au kuongezwa akiamini kama alivyousikia utapata mapokezi makubwa kwa mashabiki wa Roma ambao walimkosa kwa kipindi kirefu.

“Ninawashukuru mashabiki  kwa mapokezi makubwa tangu ulipotoka Ijumaa ya wiki iliyopita. Mimi niliupa baraka zote tangu nilipousikia kwa mara ya kwanza,” Mke wa Roma aliiambia The Playlist ya 100.5 Times Fm.

Ni siku kadhaa sasa zimepita tangu ‘Zimbabwe’ ilipotoka na Roma hajaonekana wala kuzungumza chochote juu ya Kazi yake hiyo mpya ambayo imetayarishwa na Bin Laden ndani ya Tongwe Records.

Roma amezua mijadala mingi kupitia ‘Zimbabwe’ baada ya kuweka simulizi la tukio la kutekwa kwa siku tatu na watu wasiojulikana. Hata hivyo, msanii huyo hajajitokeza hadharani kujibu maswali ya mashabiki wake kuhusu alichokiweka ndani ya ngoma hiyo.

Ndani ya muda mfupi, ‘Zimbabwe’ imeonesha kupata mafanikio makubwa kupitia mtandao wa YouTube na vyombo vya habari, ikizua mijadala mingi pia kwenye mitandao ya kijamii.

 

Video: RC Makonda atoa msaada wa miguu bandia
Mfumo washindwa kuhimili kamali ya pambano la Mayweather Vs McGregor