Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amezitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha mipango yote iliyopangwa na Serikali mwaka huu mkoani mkoani Kagera inatekelezwa kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha katika miradi yote.
 

Amesema Serikali itaendelea na mkakati wake wa kuhakikisha miundombinu yote ya usafiri na uchukuzi mkoani Kagera inajengwa kwa viwango vya juu ili kuchochea uchumi wa Mkoa huo.
 
Akizungumza mara baada ya kuanza ziara ya siku tatu Mkoani humo Prof. Mbarawa amesema Mkoa wa Kagera ni mkoa muhimu kiuchumi kwa Taifa kwa kuwa uko pembezoni mwa nchi na unaiunganisha nchi ya Tanzania na Uganda, Rwanda na Burundi ambapo ni soko zuri kwa bidhaa mbalimbali toka nchini.
 
“Tumejipanga kuhakikisha kwamba usafiri wa majini, angani na barabarani katika mkoa huu hususani kwa njia zote zinazounganisha Tanzania na Nchi jirani unaimarishwa na matokeo yake mtaanza kuyaona siku za hivi karibuni”, amesisitiza Waziri Prof.  Mbarawa.
 

 
Aidha, amesema kwa sasa Kiwanja cha Ndege cha Bukoba kitaendelea kutumika na kuboreshwa ili kiweze kutoa huduma wakati wote na kuitaka Serikali ya Mkoa wa Kagera kuhakikisha eneo lililotengwa kwa ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Omukajunguti linahifadhiwa kwa matumizi ya siku zijazo.
 
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge ameipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kuhakikisha barabara nyingi mkoani humo zinapitika wakati wote wa mwaka na kuwahakikishia kuwa mkoa huo utatoa ushirikiano kwa Wizara ili kuhakikisha miradi yote iliyopangwa kutekelezwa inakamilika kwa wakati.
 
“Mhe Waziri Mkoa wetu huu barabara  zake zikifunguka na meli ya MV Mwanza ikianza kutoa huduma uchumi wa Kagera utaimarika na kuchochea uzalishaji wa mazao ya kilimo”, amesema Meja Jenerali Mbuge.

TAMISEMI yaja na majibu ya milioni 600
Tembo aliyejifungua Pacha apewa ulinzi