Mbunge wa Tunduma kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Frank Mwakajoka amekamatwa na polisi ikielezwa kuwa atafikishwa mahakamani muda wowote kujibu tuhuma za kumpiga mtu mwaka 2018.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando amesema kuwa mbunge huyo amekamatwa na atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo za kumpiga mtu kofi, tukio alilolifanya mwaka 2018.

Amesema kuwa Mwakajoka anadaiwa kumpiga mwananchi ambaye jina lake halikutajwa na kwamba kesi hiyo imekuwa ni ya muda mrefu.

“Kuhusu jina la mtu aliyepigwa hapa sina labda unipe muda ili nilitafute, lakini mbunge Mwakajoka tunamshikilia” amesema kamanda Kyando.

Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) Mkoa wa Songwe, Ayub Sikagonamo amesema kuwa Mwakajoka amekamatwa kwa madai ya kumpiga kofi ofisa mtendaji, Deus Mwampashe.

 

Video: Aliyekataliwa na baba aongoza kidato cha 6, Wasichana wang'ara kidato cha 6 nchini
Wakulima wa kilimo cha umwagiliaji wapewa somo

Comments

comments