Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Prof. Hamisi Masanja Malebo, amepiga marufuku uuzaji wa dawa aina ya Hensha maarufu kama Mkongo na kuifutia usajili dawa hiyo inayomilikiwa na kituo cha Nyasosi Traditional Clinic cha jijini Dar es Salaam.

Prof. Malebo, ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro, na kueleza kuwa dawa hiyo imefanyiwa udanganyifu wa kiasili na kuchanganywa na dawa za kisasa za nguvu za kiume ambapo ni kinyume cha sheria.

Aidha ameeleza kuwa baraza katika uchunguzi wake, dawa hiyo yenye usajili namba TZ17TM0027, ilikutwa imechanganywa na dawa ya kisasa ya nguvu za kiume iitwayo sildenafil, kwa jina maarufu la biashara Viagra au Erecto.

Raia wavamia kambi, Wanajeshi wajeruhiwa

“Baraza pia lilibaini dawa inayoitwa Hensha alimaarufu Mkongo yenye usajili namba TZ17TM0027 ambayo ilikutwa imechanganya na dawa ya kisasa ya nguvu za kiume inayoitwa Sildenafil kwa jina maarufu la biashara ni Viagra ama Erecto kitendo hiki ni kinyume na sheria na miongozo ya usajili wa dawa za tiba asili na mbadala,” amesema Prof Malebo.

“Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, kuanzia leo tarehe 27 Julai, 2022 limefuta usajili wa dawa ya Hensha alimaarufu Mkongo inayomilikiwa na kituo cha Nyasosi Traditional Clinic na ihakikishe dawa hiyo inaondolewa sokoni mara moja kuanzia leo vinginevyo hatua kali ya kisheria itachukuliwa dhidi ya Bw. Emmanuel Maduhu,” amesisitiza.

Prof. Malebo, amesema kitendo hicho ni kinyume cha sheria na miongozo ya usajili wa dawa za tiba asili na mbadala na kimetakiwa kuhakikisha kinaiondoa sokoni mara moja dawa hiyo, vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mmiliki.

Pia, Prof. Malebo ameweka wazi kuwa, Kwa mganga ambaye anahitaji kutangaza dawa yake ni lazima afuate utaratibu wa kusajili dawa kwa kupima ubora na usalama na baadaye aombe kibali cha matangazo kutoka Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.

Sambamba na hilo Prof. Malebo amesema, Baraza lilifanya uchunguzi na kubaini baadhi ya dawa kuwa na mapungufu madogo hasa kwenye uandishi wa lebo na vifungashio, na dawa mbili zilibainika kuwa na kiashiria cha hali duni ya usafi wa mazingira ya kutengenezea dawa hizo.

Vile vile, Prof. Malebo amesema, Baraza linaendelea kuwakumbusha wananchi kupata huduma kwa waganga na vituo ambavyo vimesajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na kutumia dawa asili ambazo zimepimwa ubora na usalama pamoja na kusajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.

Simba SC yapigika Misri
Majeruhi ajali ya King David wapewa rufaa