Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) George Mkuchika ameahidi kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale waliotumia vibaya fedha za miradi ya maendeleo na kupelekea kutomalizika kwa miradi hiyo.

Ameyasema hayo wilayani Liwale wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo mkoani Lindi, kabla ya kutembelea utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na TASAF wilayani humo.

Amewataka watumishi wote wanaojijua kuhusika na ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo kuzirudisha mapema kabla majina yao hayajafikishwa ofisini kwake.

Aidha, amefafanua kuwa, Serikali imekuwa ikipeleka fedha za miradi ya maendeleo kila wilaya mkoani Lindi ili kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwezo zahanati, vituo vya afya, umwagiliaji na ujenzi wa barabara lakini fedha hizo zimeonekana kutumika vibaya kwani miradi haijamalizika lakini fedha zimeisha.

Vile vile ameainisha kuwa, taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Liwale inaonyesha Halmashauri hiyo inadaiwa takribani shilingi milioni 465 hivyo kupelekea kuzorota kwa uchumi wa Wilaya hiyo kutokana na makusanyo ya fedha kuishia kulipa madeni yanayotokana na matumizi mabaya ya fedha.

Hata hivyo, Mkuchika amewataka watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Liwale kuridhika na mishahara yao na kuacha kuomba rushwa kutoka kwa wananchi wanapohitaji huduma kwani kwa kufanya hivyo, kunawanyima wananchi haki yao ya kupata huduma.

 

Paka arithi mabilioni ya fedha
Video: Rais Trump adata na danadana za mwanamke Mtanzania, afunguka