Kiungo wa mabingwa wa soka Tanzania bara Wekundu Wa Msimbazi Simba Jonas Mkude, amesema kuwa endapo Ligi Kuu Bara itaendelea baada ya kusimama kwa muda, kutakuwa na changamoto mbalimbali kwa wachezaji kurejea kwenye ari ya mchezo ikiwamo suala la kukosa pumzi na majeraha.

Mkude ametoa kauli hiyo wakati huu kukiwa bado haifahamiki ni lini ligi itarejea kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Corona.

Fundi huyo wa mpira amesema changamoto kubwa anayoiona iwapo wachezaji watarejea ni kwamba wengi wao watakabiliwa na suala la uwiano tofauti wa pumzi ikiwamo baadhi yao kukata mapema, jambo ambalo litaziathiri timu nyingi katika juhudi za kusaka ushindi.

Aidha, Mkude aliongeza kuwa kutokana na kila mtu kufanya mazoezi kivyake haamini kama kila mmoja anajibidiisha kuyafanya ipasavyo huko aliko kwa sasa.

Ligi mbalimbali za soka duniani zimesimama kupisha juhudi za kukabiliana na ugonjwa wa Corona ambao umekuwa changamoto na kusababisha mambo mengi kusimama.

Ligi ya soka Tanzania bara imesimama huku Simba SC wakiwa wanaongoza kwa alama zao 71, wakifuatiwa na Azam FC alama 54 baada ya wote kucheza michezo 28, wakati vigogo Young Africans ni wa tatu kwa alama zao 51 za michezo 27 na Namungo wa nne wakiwa na alama 50 za michezo 28.

Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa alama zake 15 za michezo 29, nyuma ya Mbao FC wenye alama 22 za michezo 28, Alliance FC alama 29, michezo 29, Mbeya City alama 30 michezo 29 na Ndanda FC alama 31 michezo 29.

Mkuu wa ujasusi awa Waziri mkuu mpya Iraq
WHO wamjibu Trump, "hatuna upendeleo"