Saa chache baada ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuzuia kufanyika kwa Tamasha la Fiesta leo usiku katika viwanja vya Leaders Club jijini humo, Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Aron Kagulumjuli ameeleza madhara yalisababisha hatua hiyo.

Kagulumjuli amesema kuwa sauti ya muziki ya tamasha hilo, ilikuwa hatari kwa maisha watu wengine hususan wagonjwa walio katika hospitali zilizoko jirani. Alisema kuwa jana walipokuwa wanafunga jukwaa na vifaa pamoja na kufanya majaribio, watu wawili walizimia.

“Jana tu walipokuwa wakitangaza hapo Leaders, maeneo ya karibu kuna hospitali na watu wawili walizimia. Kwa njia hiyo, hatuwezi kuruhusu furaha ya watu wengi ikawa majonzi kwa wengine,” Mwananchi wanamkariri Kagulumjuli.

Aliongeza kuwa wameamua kusitisha tamasha hilo kufanyika katika viwanja hivyo, hadi watakapojiridhisha kuwa kuna usalama kwa watu wengine.

Katika barua yao, iliyoandikwa na ofisa utamaduni wa halmashauri ya manispaa hiyo, ilieleza kuwa wamezuia kuanyika kwa tamasha hilo katika viwanja hivyo na kuelekeza tamasha hilo lifanyike katika viwanja vya Tanganyika Packers.

Kufuatia katazo hilo, kamati ya Maandalizi ya Fiesta imetangaza kuahirisha tamasha hilo na kurudisha fedha kwa watu waliokuwa wamenunua tiketi.

Tamasha hilo linaloandaliwa na Clouds Media Group, lilikuwa linafikia kilele chake leo jijini Dar es Salaam, baada ya kuzunguka katika mikoa 14. Kwa miaka kadhaa, tamasha hilo limekuwa likihitimishwa katika viwanja vya Leaders Club, ingawa mwaka jana kulikuwa na sintofahamu ya muda wa kumalizika kwa tamasha hilo.

Majiji ya Arusha na Dodoma vinara ukusanyaji mapato
Rais Shein afungua jukwaa la biashara Zanzibar, Asisitiza utoaji huduma bora