Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Jumanne Mei 24, 2022 amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt. John Pima na maafisa wengine sita kwa makosa ya matumizi mabaya ya fedha na tuhuma za kughushi nyaraka.

Watumishi wengine waliosimamishwa kazi ni mweka Hazina wa Jiji Mariam Mshana, Innocent Maduhu, Alex Tlehama, Nuru Gana wote kutoka ofisi ya mchumi na Afisa Manunuzi Joel Mtangi ambaye alihamishiwa kikazi Halmashauri ya Wilaya ya Longido.

“Hatuwezi kuvumilia kuona fedha za umma zinapotea kienyeji hawa watumishi watakaa pembeni kupisha uchunguzi hadi kazi hiyo itakapokamilika Kamanda wa TAKUKURU  fuatilia hadi ijulikane ni akina nani waliohusika,” ameagiza Majaliwa.

Amesema Mkurugenzi anatuhumiwa kwa kutosimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi ya maendeleo na matumizi mabaya ya vifaa vya ujenzi ambavyo vilipelekwa kwenye nyumba binafsi iliyoko Olkereyan eneo la Njiro chini ya usimamizi wa Joel Mtango.

“Nondo, matofali, misumari, mbao, gypsum boards, saruji, mchanga, kokoto na bati vyenye thamani ya shilingi milioni 44 viliagizwa kupitia kampuni ya cherry general supplies and services na kupelekwa kwenye nyumba binafsi iliyoko Olkereyan Njiro,” amefafanua.

Aidha amefafanua kuwa Machi 28, 2022 Mkurugenzi alimuagiza mweka Hazina aingize shilingi milioni 103 kwenye akaunti binafsi ya Innocent Maduhu kwa ajili ya shughuli za kiwanda cha matofali na kuhoji iweje fedha ya kazi iingizwe.kwenye akaunti ya mtumishi binafsi badala ya akaunti za Kata.

“Tarehe 14 Aprili, 2020 uliagiza milioni 65 ziingizwe kwenye akaunti ya Alex Daniel zikiwa ni malipo kwa ajili ya matenegenezo ya barabara za kata na mitaa na tarehe hiyo hiyo shilingi milioni 65 ziliingizwa kwa Nuru Ginana zikiwa ni malipo ya kununua molamu jumla ni shilingi milioni 233 ambazo hazikutumika kwa lengo lililokusudiwa,” amesema.

Mkurugenzi huyo pia anatuhumiwa kuhamisha watumishi 50 kati ya Januari na Mei 2022 na kumuomba mmiliki wa kampuni ya Cherry General Supplies awape risiti ya shilingi milioni 103 hali iliyosababisha adaiwe milioni 15 na TRA fedha ambazo hakuwa nazo na akatishiwa kushtakiwa.

Waziri Mkuu pia amebaini mabati yaliyotumika kwenye ujenzi wa vibanda vya wamachinga ni ya geji 30 wakati kanuni zinataka majengo yote ya Serikali yatumie mabati ya geji 28.

Akiwa mkoani Arusha kwa ziara ya siku moja Waziri Mkuu amekagua masoko ya Mbauda, Kilombero na Machame na kuzungumza na baadhi ya wamachinga wanaofanya biashara kwenye masoko hayo na baadae kufanya kikao na Viongozi wa jiji katika ukumbi wa mikutano wa AICC.

Spika:Marufuku vituko bungeni
Diwani aliyepotea akutwa nyumbani kwa mwanamke