Kamati Tendaji ya Chama Cha Mpira wa Miguu Tanzania (ZFA), imemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama hicho, Masoud Attai  aliyekuwa akihusika na shughuli zote za kiufundi za soka ikiwa ni pamoja na kozi mbalimbali za makocha na miradi ya soka ya vijana ktuoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Kamati hiyo imechukua uamuzi huo ikiwa ni siku chache baada ya kuchukua nafasi ya Kamati ya mpito iliyokuwa ikiongoza chama hicho. Attai ndiye mtayarishaji na mtunzaji mkuu wa ratiba za ligi na mashindano yote yanoyoendeshwa na chama hicho.

Akizungumza kwa niaba ya kamati Kamati Tendaji, Mussa Suleiman Soraga ambae ni mjumbe wa ZFA Taifa akitokea Wilaya ya Magharibi “A”, alisema wamemsimamisha kwa makosa kadhaa yakiwemo kuratibu mafunzo ya leseni kwa vilabu ambapo alivishirikisha vilabu ya Unguja tu pekee wakati vya kisiwani Pemba hajavishirikisha katika kozi hiyo.

“Tumemsimamisha Attai kutokana na agizo tulolijadili kwenye kikao cha dharura kwenye mkutano mkuu kwasababu aliendesha kozi ya Leseni kwa vilabu ambapo alivishirikisha vilabu vya upande mmoja tu wa Unguja wakati vilabu vya Pemba havijashirikishwa na ile kozi ni muhimu kwa timu zote za ligi kuu Zanzibar,” Soranga anakaririwa.

Aidha Soraga alisema Attai ana makosa mengine ya kubadilisha mtandao wa ZFA mara kwa mara kwa maslahi yake binafsi.

“Kosa lake jengine huwa anabadilisha mtandao wa ZFA mara kwa mara kwa maslahi yake binafsi ambapo sisi huwa tunapata tabu kufanya mawasiliano na CAF na sehemu nyengine”.Alisema Soraga.

Baada ya hivi karibuni mkutano mkuu wa chama hicho kumpiga shoka la shingo Makamu Urais ZFA Unguja Alhaj Haji Ameir (Mpakia) na kuvunjwa kamati ya muda iliokuwa ikisimamia shughuli za ZFA ikiwemo kuendesha ligi kuu soka Zanzibar kanda ya Unguja, hivi sasa Kamati Tendaji ya ZFA Taifa imeunda kamati mpya itakayosimamia ligi kuu soka Zanzibar kanda ya Unguja yenye wajumbe 7 ambapo mwenyekiti wa kamati hiyo Mohd Ali (Tedy) na katibu wake Hashim Salum wakiwemo wajumbe wengine Abdallah Thabit (Dula Sunday), Haji Issa Kidali, Hussein Ali Ahmada, Vuai A Vuai na Ali Bakar (Cheupe)

 

 

Maalim Seif atoa ya moyoni baada ya kutoka Hospitali
Yanga Yaishushia African Sports Kichapo Cha Paka Mwizi