Mkutano wa kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi – COP27, unaanza hii leo Jumapili Novemba 6, 2022 katika mji wa mwambao wa bahari ya Sham wa Sharm el-Sheikh nchini Misri.

Mkutano huo, unatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya wawakilishi wa nchi 200 Duniani, ukilenga kujaribu kwa mara nyingine kuona jinsi ya kushughulikia taathira za mabadiliko ya Tabianchi wakati huu mambapo ulimwengu ukikabiliwa na vita na mzozo mkubwa wa kiuchumi.

Tangazo la mkutano wa kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP27. Picha ya Sayed Sheasha/ Reuters.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ametahadharisha kuwa, Dunia inaelekea katika hali isiyorekebishika ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kufuatia hatua hiyo, Guterres amewahimiza viongozi watakaohudhuria mkutano huo kuuweka ulimwengu katika njia sahihi ya kupunguza gesi zinazochafua mazingira, na kutimiza ahadi zao za ufadhili kusaidia nchi maskini kutumia nishati safi.