Mkutano Mkuu wa kawaida wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) uliokuwa ufanyike Tanga ikiwamo shughuli ya uwekaji jiwe la msingi kwenye kiwanja cha TFF jijini Tanga umeahirishwa kwa muda usiojulikana.

Mwishoni mwa mwezi Novemba 2015, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) mkoa wa TRA wa Ilala ulitoa agizo la kufungwa na kuchukuliwa fedha kutoka kwenye akaunti za TFF ili kulipa fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.6, sehemu kubwa ikiwa ni malipo ya kodi kutoka kwenye mishahara (PAYE) ya makocha Jan Poulsen, Kim Poulsen, na Jacob Michelsen na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye mchezo kati ya Tanzania na Brazil mwaka 2010.

Baada ya hatua hiyo TFF iliwasiliana na TRA na kuweka bayana kwamba deni la walimu (makocha) na mchezo dhidi ya Brazil lilistahili kulipwa na serikali na haikuwa sahihi kulielekeza TFF.

Aidha,  TFF ilieleza athari ambazo zingetokea iwapo amri hiyo (Agent Order) ingetekelezwa kuwa ni pamoja na kusitishwa kwa ziara ya timu ya vijana chini ya miaka 15 (U15) katika nchi za Rwanda, Uganda na Kenya, kusimama kwa program za vijana na wanawake, Mkutano Mkuu, Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Kombe la Shirikisho.

Baada ya utekelezaji wa amri hiyo kuanza TFF ilifanya kikao na TRA na makubaliano ya kufungua akaunti yakafanikiwa.

Hata hivyo,  akaunti zilifunguliwa zikiwa hazina fedha kwa kuwa zilishapelekwa Benki Kuu (BOT) na zoezi la madai lisingeweza kukamilika kwa muda mfupi.

Baada ya hali hiyo kujitokeza, TFF ilifanya kila linalowezekana kuhakikisha Mkutano Mkuu unafanyika ikiwa ni pamoja na kutafuta ufadhili toka kwa  wadau wake, lakini zoezi hilo limeshindikana katika muda mfupi uliopo na hivyo Shirikisho  limeamua kuahirisha Mkutano Mkuu 2015 mpaka hapo hali itakaporuhusu.

Rais Magufuli Amuondoa Dk. Hoseah Takukuru, amteua huyu
Utafiti: Uongozi wa Nchi Hupunguza Umri wa Kuishi, Hatari kwa Afya