Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo amefanya kikao na Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani humo kuhusu matukio ya mauaji ya watoto yaliyoanza Novemba mwaka jana.

Jenerali Mabeyo ambaye ni Mwenyekiti wa vyombo vyote vya ulinzi na usalama amesema kuwa yuko mkoani humo kwa ajili ya kufuatilia maendeleo ya zoezi la kukabiliana na matukio hayo kwakuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinashirikiana.

“Vyombo vyote vya ulinzi na usalama vinafanya kazi kwa kushirikiana ikiwa ni pamoja na jeshi. Na mimi kama Mwenyekiti wa vyombo vyote vya ulinzi na usalama ninao wajibu na sio kwamba jeshi limeingia sasa, hapana hatujafikia hatua ya kuingiza jeshi,” alisema Jenerali Mabeyo katika kikao kati yake na Kamati ya Ulinzi na Usalama kilichofanyika leo.

Alisema kuwa taarifa za mauaji ya watoto mkoani humo zimesambaa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania na kuzua hofu kwa raia, na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vilituma vikosi maalum mapema kwa ajili ya kushirikiana na vikosi vya mkoani humo kufanya uchunguzi wa kina.

Aidha, Jenerali Mabeyo alisema kuwa suala la mauaji hayo limeanza kubainika kuwa ni la kifamilia kwani linahusisha familia moja moja na sio la kitaifa, hivyo alisema lazima itafutwe njia ya kuyakomesha.

Amewataka wananchi kuendelea kufanya kazi zao kwani vyombo vya dola vinaendelea kutekeleza wajibu wake wa ulinzi na usalama, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wahusika wa matukio hayo.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Mkoani Njombe, hadi sasa watu 30 wanashikiliwa wakihusishwa na matukio hayo ya mauaji ya watoto.

Mswada wa sheria ya vyama vya siasa wawakosha wabunge CCM
Viongozi CCM wataka mauaji ya watoto Njombe yasitumike kisiasa.