Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala ameagiza kusitishwa kwa matumizi ya vifungashio vya plastiki visivyokidhi viwango, kwani matumizi yake yamekuwa chanzo cha uchafuzi wa mazingira.

Makalla, ameyasema hayo katika kikao na Wadau wa Taasisi mbalimbali za Serikali likiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na usimamizi wa Mazingira (NEMC), Shirika la kudhibiti ubora na viwango Tanzania (TBS), Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Polisi na Wawekezaji wanaozalishaji wa mifuko mbadala.

Amesema, “Naelekeza kikosi kazi kuanza operesheni katika Mkoa wa Dar es Salaam, kuondoa vifungashio vya plastiki visivyokidhi viwango ambavyo imegeuzwa kuwa mifuko ya kubebea bidhaa katika masoko yote.”

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala.

Aidha, ameiagiza NEMC kuandaa kikao na Wenyeviti na Makatibu wa Masoko katika mkoa huo, ili kuwapa elimu kuhusiana na matumizi ya vifungashio visivyokidhi viwango katika maeneo ya masoko Mkoani Dar es Salaam.

Makalla ameongeza kuwa, baada ya kikao hiko NEMC ianze oparesheni ya kutokomeza vifungashio hivyo vya plastiki visivyokidhi viwango mara moja na wote wanaotumia vifungashio hivyo visivyokidhi viwango wachukuliwe hatua za kisheria.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Samuel Gwamaka akiongea katika kikao hiko amemshukuru Mkuu wa Mkoa kuwaomba na Wakuu wengine wa Mikoa kuiga mfano huo ili kuweza kurahisisha zoezi hilo la kutokomeza vifungashio visivyokidhi viwango.

Kata hivyo, ameainisha changamoto ambazo NEMC inakutana nazo katika kutokomeza vifungashio vya plastiki visiyokidhi viwango, ikiwemo njia za panya za uingizaji wa mifuko hiyo na kupata ushirikiano mdogo kutoka serikali za mitaa kuanzia ngazi ya chini.

Naye, Mkurugenzi wa Udhibiti wa viwango kutoka TBS, Lazaro Henry Msasalaga amesema Shirika la Viwango liko tayari kushirikiana na NEMC kama walivyofanya awali, ili kuweza kutokomeza vifungashio visivyokidhi vigezo.

Rais Samia amteua Prof. mwandosya
Kenya: Dua la Kuku linavyoweza kumpata Mwewe