Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba juzi alikutana na changamoto ya aina yake baada ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose Nyamubi kumkataza kufika majira ya usiku katika kijiji kimoja cha wilaya hiyo kilicho na mgogoro wa ardhi kwa miaka 30 hadi sasa.

Mkuu huyo wa Wilaya alimueleza Waziri Nchemba kuwa kijiji cha Mikomario kina wanakijiji wakorofi hivyo sio eneo salama kwa kiongozi huyo kufika majira ya usiku kutokana na mgogoro wa ardhi uliopo.

Hata hivyo, Waziri Nchemba alisisitiza kuwa ni lazima afike kwenye eneo hilo ingawa alifahamu atafika majira ya usiku kwani aliwaahidi wanakijiji hao kuwa atafika na walikuwa wakimsubiri yeye tangu mchana.

Mkuu wa Wilaya aliweka wazi kuwa endapo ataelekea kwenye kijiji hicho, yeye hatawajibika na lolote la kiusalama litakalotokea na hatajihusisha na kikao hicho.

Taarifa kutoka wilayani humo zinaeleza kuwa Nchemba alifanikiwa kufika katika kijiji hicho majira ya saa moja kasoro na kufanya mkotano na wananchi hao huku Mkuu huyo wa Wilaya akijitenga na kutokaa kwenye meza kuu.

“Suala hili ni la kisheria, kwahiyo linatakiwa kutatuliwa kisheria na sio mapigano. Nipeni fursa ili wizara yangu iwasiliane na wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na TAMISEMI  ili kuweze kuutafutia ufumbuzi kwa pamoja,” alisema Nchemba.

Wananchi hao walionesha kufurahishwa na maelezo na ujio wa Waziri huyo na aliondoka kwa usalama usiku huo akiwaacha na matumaini mapya.

 

Jerry Muro atuhumiwa kuwalaghai wachezaji wa Simba
Ukawa wawapooza waathirika wa ‘Bomoabomoa’