Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa ‘Master’ amekiri Simba ya msimu huu ni moto wa gesi na kuongeza kuwa ina sababu zote za kuweza kufanya vizuri zaidi, ikiwezekana kuchukua ubingwa, lakini akasisitiza sana juu ya safu yao ya ushambuliaji.

Mkwasa ameyasema hayo baada ya kuishuhudia Simba ikichomoza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es salaam, mwishoni mwa juma lililopita.

“Simba ina kikosi kizuri, karibu imekamilika kila idara, kuanzia golini mpaka kiungo iko vizuri sana na inacheza kwa kuonana, lakini sema bado wana tatizo kwenye safu ya ushambuliaji.

Wapo baadhi wanakwamisha mbinu za mwalimu, wanaonekana kila mmoja anataka afunge mwenyewe hata kama hayupo kwenye nafasi ya kufunga.

Hili ndilo tatizo kubwa kwa timu yao. Sitawataja lakini wapo na ni tatizo kwa timu yao.

“Nafikiri kocha wao akifanikiwa kulitatua, iwe ni kuelewana ama kukemea naamini Simba inaweza kufanya kitu cha ajabu msimu huu,” alisema kocha huyo ambaye aliwahi kuvinoa vikosi vya Yanga na Ruvu Shooting.

Licha ya kutowataja lakini tunafahamu aliwalenga zaidi Fredric Blagnon na Laudit Mavugo ambao mara kadhaa kumekuwepo na malalamiko juu yao kwa umimi kama ilivyotokea kwenye mchezo wa juzi.

Ushindi huo uliifanya Simba iendelee kung’ang’ania kileleni kwa kufikisha pointi 23 huku kichapo kikiiacha Kagera na pointi zao 13.

Mfumo Wa Hans Pluijm Wamkimbiza Malimi Busungu
ATCL Yatoa Ofa ya Mwezi Mmoja