Kocha wa muda wa klabu ya Young Africans Boniface Mkwasa, ameendelea kusisitiza suala la kutengeneza mfumo mpya, utakaokiwezesha kikosi chake kupambana vilivyo kwenye michezo ya ligi kuu, katika muda wote atakaoendelea kuwepo kwenye benchi la ufundi.

Mwishoni mwa juma lililopita, Young Africans walipata ushindi wa mabao matatu kwa moja dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa kirafiki, ambao ulitumiwa na kocha Mkwasa kujiandaa na michezo ya ligi kuu itakayoendelea mwishoni mwa juma hili.

Mkwasa amesema lengo lake kubwa ni kutaka kuona kiksoi cha Young Africans kikicheza soka la ushindani, na kikiwa kwenye mfumo tofauti na ilivyokua, kabla hajakabidhiwa jukumu la kukalia benchi la ufundi kwa muda.

Amesema anataka kuona timu ikishindana wakati wote, na kuwafurahisha mashabiki, ambao siku zote wamekua wakiamini wana kikosi bora, ambacho kina uwezo wa kushindana na yoyote ndani na nje ya nchi.

“Kabla sijateuliwa kuwa kocha wa muda, Young Africans ilikua ikicheza soka la kujihami kwa asilimia kubwa, katika utawala wangu sitaki iwe hivyo, kwa sababu tukiendelea kufanya hivyo tutakua dhaifu, inampasa kila mchezaji kubadilika na kutambua mfumo ambao ninataka wacheze ndani ya dakika 90,” amesema Mkwasa.

“Hii timu ni ya mashabiki ambao siku zote wamekua wanakuja uwanjani kwa ajili ya kuangalia soka ambalo litachagizwa na ushindi, haipendezi watu wanakuja kwa ajili ya timu yao halafu wanashuhudia mchezo wa kujihami kwa kiasi kikubwa, yatupaswa kupambana na yoyote kwa soka la kushambulia na wakati fulani tujihami, inapobidi.” Aliongeza Mkwasa.

Mkwasa aliteuliwa kuchukua majukumu ya kuwa kocha wa muda klabuni hapo, baada ya kutimuliwa kwa kocha kutoka DR Congo Mwinyi Zahera, ambaye hakufanikiwa kushinda taji lolote tangu alipowasili msimu uliopita.

Tayari Mkwasa ameshakishuhudia kikosi chake kikipambana kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ndanda FC ambao walikubali kulala kwa bao moja, kwenye uwanja wao wa nyumbani (Nangwanda Sijaona) mjini Mtwara.

Mwishoni mwa juma hili Young Africans wataendelea na mshike mshike wa ligi kuu ya soka Tanzania bara kwa kupapatuana na maafande wa jeshi la kujenga taifa JKT Tanznaia, kwenye uwanja wa Uhuru, jijini Dar es salaam.

Mahiga aitaka THBUB kuimarisha utawala bora
Simba SC wathibitisha kuondoka kwa Patrick Aussems