Mahakama kuu kanda ya Moshi imemhukumu adhabu ya kifo aliyekuwa mlinzi wa shule ya sekondari ya Scolastica, Hamisa Chacha baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumuua kwa kukusudia aleyekuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule hiyo, Humphrey Makundi (16) aliyeuawa Novemba 6 mwaka 2017.

Pia mahakama hiyo imewahukumu kifungo cha miaka minne kila mmoja, mmiliki wa shule hiyo, Edward shayo pamoja na aliyekuwa mwalimu wa nidhamu, Labani Nabiswa, baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la kushiriki jinai baada ya tukio la mauaji huku ikiwafutia kosa la mauaji ya kukusudia.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Frimin Matogolo, amesema mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ambaye ni mlinzi ametiwa hatiani kwa kosa la kuua kwa kukusudia chini ya kifungu cha sheria namba 196 cha kanuni ya adhabu ambapo amesema kwa maelezo ya ungamo yaliyotolewa na mshtakiwa huyo mbele ya mlinzi wa amani yanatosha kumtia hatiani.

Jaji Matogolo ameeleza kuwa ushahidi wa mshtakiwa wa kwanza kwenda kuonyesha silaha ambayo ni panga alilotumia kuua unatosha kumtia hatiani pia katika kosa hilo la mauaji ya kukusudia.

Kutokana na hilo Jaji Matogolo amesema kosa hilo la kuua kwa kukusudia lina adhabu moja ya kunyongwa hadi kufa na kwa mujibu wa sheria namba 167 ya kanuni ya adhabu mahakama hiyo inamhukumu kunyongwa hadi kufa.

Na upande wa mshtakiwa wa pili ambaye ni mmiliki wa shule ya Scolastica,Edward Shayo pamoja na mshtakiwa wa tatu ambaye ni mwalimu wa nidhamu, Labani Nabiswa, Jaji amesema wao walishiriki katika kutupa mwili wa marehemu Humphrey Makundi mtoni lakini hakuna ushahidi unaoonesha wameshiriki kufanya mauaji.

Jaji Matogolo ameongeza kuwa kosa walilotiwa hatiani nalo lina adhabu ya kifungo kisichopungua miaka saba jela, lakini kutokana na maombi yaliyotolewa na mawakili wao mahakama imewahukumu kutumikia kifungo cha mika minne jela.

 

 

 

Bei ya mahindi Kenya yapaa, Viwanda 10 vyafungwa
Gumzo laibuka ziara ya Rais Trump London