Vanessa Mdee amefafanua kauli yake ya kuacha muziki aliyoitoa hivi karibuni, akieleza kuwa imetokana na ‘mauzauza’ aliyokutana nayo kwenye tasnia ya muziki, kiasi cha kuhoji wanaotaka aendelee wanataka afe?

Akizungumza jana jioni kupitia akaunti yake ya YouTube, Vanessa alisema kuwa kiwanda cha muziki kilimfanya aishe maisha magumu sana kiasi cha kupata msongo wa mawazo na huzuni kubwa mara kwa mara.

Alisema kuwa ingawa watu huwaona wasanii wakiwa na furaha kupitia mitandao ya kijamii, hali iko tofauti sana kiuhalisia kwani wengi wana maumivu moyoni wanayopitia hadi kuvuna matunda madogo ya kazi zao.

Vanessa ambaye hivi sasa yuko ughaibuni, alisema kuwa hawezi kuacha kuimba na kufanya matamasha kwakuwa ndio sehemu ya maisha yake, lakini hatajihusisha moja kwa moja na kiwanda cha muziki au tasnia ya muziki kama alivyofanya awali.

Msanii huyo wa kike ambaye kabla ya kuanza muziki alikuwa mtangazaji, ametoa mfano wa mkulima ambaye amekuwa akivuna mazao yake vizuri hata mara mbili kwa mwaka na watu wakamsifu, lakini ndani ya kipindi cha kuandaa shamba hadi mavuno anakuwa amepitia mateso makubwa kiasi cha kushindwa kufurahia kwa dhati mavuno aliyonayo.

Amesema mkulima ndiye unayefahamu anayopitia hadi kupata mazao hayo yanayosifiwa sokoni, lakini kama anapitia mfumo uleule wa mateso kila mwaka uvumilivu utakushinda.

“Niko kwenye muziki kwa miaka 13, lakini nimefanya muziki kwa miaka saba na kila mwaka narudia mfumo uleule, lakini nimekuwa ninafanya kwa kujificha. Sasa, kwa kuficha nimekuwa ndani naumia. Nataka kumridhisha kila mtu kuanzia mashabiki hadi makampuni ninayofanya nayo kazi, lakini mimi sina raha, sina furaha kila siku naingia shambani nang’atwa na nyoka, mavuno ni mazuri lakini mateso ni makubwa,” alisema Vanessa.

Msanii huyo ambaye albam yake ya Money Mondays imevunja rekodi ya kuwa albam iliyosikilizwa na kupakuliwa mara nyingi zaidi mtandaoni kwa Afrika Mashariki, alisema kuwa anaelewa kila biashara ina changamoto, lakini biashara nyingi zenye changamoto tofauti na ilivyokuwa kwenye muziki zinatoa ahadi na matumaini ya kubadilika siku za usoni.

Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo, alikuwa anapata matatizo ya afya ya akili ambayo yamesababisha madhara makubwa.

“Watu wengi hawawezi kuelewa mental health (afya ya akili), sio kitu ambacho waafrika tunaona kama kina umuhimu, kama akili yako haiko sawa, kuna msongamano wa mawazo… kama una msongo wa mawazo, una presha nyingi, inakuweka katika nafasi ambayo hauna furaha na maisha yako na huwezi kuendelea mbele wala kufanya kitu chochote,” alisema.

“Kwahiyo, unakuwa unatembea tu kama roboti unafanya vile vitu unavyotakiwa kufanya kwa sababu ni kazi,” Vee Money aliongeza.

Alizungumzia pia mitazamo ya watu wengi kwenye mtandao wa kijamii wanaomsihi kutoachana na kiwanda cha muziki.

“Kuna mitazamo mingi sana [kuhusu kuachana na tasnia ya muziki]. Je, mgependa kusikia baada ya miezi au miaka kadhaa ‘Vanessa alikufa’, au ‘Vanessa alipata majeraha zaidi ya kiafya na kimwili na kiakili’. Kwa sababu gani, hatujui,” Vanessa amefunguka zaidi.

Mkali huyo wa ‘Bambino’ alisema kuwa ni dhahiri kuwa kila mtu anaonja umauti, lakini kuna vitu vingine vinaweza kuepukika na amechagua kuviepuka.

Katika hatua nyingine, Vanessa alieleza kuwa baada ya kupata nafasi ya kuwa chini ya lebo ya Kimataifa ya ‘Universal Music Group’, alijua atapiga hatua kubwa sana ikiwa ni pamoja na kuongeza nafasi ya kuuza kazi zake duniani. Anasema alichokiona baada ya kufanya kazi na lebo hiyo ni bora angeendelea kufanya kazi mwenyewe kwani ahadi zilikuwa nyingi na kubwa lakini kwenye utekelezaji ni mitihani mikubwa.

Msanii huyo hivi sasa anafanya kazi na lebo yake ya ‘Mdee Music’. Amesisitiza kuwa ataendelea kufanya nyimbo na kutumbuiza lakini hatajihusisha moja kwa moja na tasnia ya muziki.

Vanessa alianza kung’aa kwenye kiwanda cha muziki baada ya kuachia wimbo wa ‘Closer’ alioutoa mwaka 2013 akiwa chini ya lebo ya ‘B’Hitz’, wimbo ambao ulimpa tuzo.

Alianza muziki kama rapper, akabadili gia angani na kuwa muimbaji aliyepata nafasi kwenye anga la Kimataifa. Nyumbani alifanya ziara kubwa akiwa na mpenzi wake Jux, iliyoitwa ‘In Love and Money’.

Vurugu za Mashabiki wa Yanga zauibua uongozi

Ajira: Makampuni 10 yatangaza nafasi za kazi, ziko hapa

Mourinho azungumzia tuhuma za kuua vipaji
Vurugu za Mashabiki wa Yanga zauibua uongozi