Mmiliki wa klabu ya Newcastle Utd, Mike Ashley anaamini kikosi cha klabu hiyo kitafaulu mtihani wa kubaki katika ligi kuu ya soka nchini England, chini ya utawala wa meneja kutoka nchini Hispania, Rafael Benitez.

Ashley, ametangaza imani yake kwa Benitez, alipohojiwa na kituo cha televisheni cha Sky Sports, ambapo amesema hana shaka na uwezo wa meneja huyo, ambaye siku zote amekua mpambanaji katika hatua ngumu kama inayowakabili kwa sasa.

Ashley ambaye alifanya maamuzi ya kumtimua, Steve McLaren majuma mawili yaliyopita na kumkabidhi kikosi Banitez, amesema kwa sasa ameanza kuona mwangaza wa mafanikio, kutokana na matokeo ya sare ambayo yalipatikana mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Sunderland.

Mmiliki wa klabu ya Newcastle Utd, Mike Ashley

Kibopa huyo pia anaamini uwepo wa mshambuliaji Aleksandar Mitrovic, ambaye alimsajili kwa ada ya uhamisho wa paund million 13, akitokea R.S.C. Anderlecht mwaka 2015, pia kunamuaminisha mambo yatakaa sawa.

Mitrovic, alifunga bao la kusawazisha mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Sunderland, na kuwafurahisha mashabiki wengi wa The Magpies ambao walikua wameshaanza kuonyesha hali za huzuni wakati mchezo huo ulipokua ukiendelea.

Aleksandar Mitrovic celebrates his goal for Newcastle against SunderlandMshambuliaji Aleksandar Mitrovic, akishangilia baada ya kufunga bao la kusawazisha wakati wa mchezo dhidi ya Sunderland

Mpaka sasa Newcastle Utd, imeendelea kukaa kati nafasi ya pili kutoka mkiani mwa msimamo wa ligi ya nchini England, hali ambayo bado inatoa nafasi kwa kila mmoja klabuni hapo kuamini watafanikiwa kubaki katika ligi kuu msimu wa 2016-17.

Mchezo ujao Newcastle Utd, watapambana na Norwich City ambao wapo katika nafasi ya 17 katika msimamo wa ligi kuu ya soka nchini England, kwa kufikisha point 28 ikiwa ni tofauti ya point tatu dhidi ya vijana wa Benitez.

Kama Newcastle Utd watafanikiwa kuibuka na ushindi katika mchezo huo, watajiondoa katika orodha ya timu ambazo zipo katika mstari wa kushuka daraja kwa msimu huu.

Nigeria Wakamilika Kambini, Kuwavaa Misri March 25
Chris Coleman: Ni Marufuku Wachezaji Kusafiri Na Wake Zao