Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amerejea nyumbani baada ya ziara yake nchini Urusi, kufuatia vurugu za maandamano zilizosababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta.

Serikali ya Zimbabwe imekuwa ikiulaumu upinzani kutumia hali ya kupanda kwa bei ya mafuta nchini humo, kuchochea ghasia na maandamano.

Aidha upinzani umesema kuwa wanachama wake wamekuwa wakichukuliwa hatua kali kama hatua ya kujibu vurugu za maandamano yanayofanywa kupinga ongezeko la bei ya mafuta.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC), Nelson Chamisa amesema kuwa wanachama wao wamekamatwa wakiwemo wabunge watano, huku afisa wake mwingine mwandamizi akiwa amejificha.

Makundi ya haki za binadamu yamesema kuwa watu 12 wameuawa katika ghasia hizo. huku mengine yakisema kuwa idadi hiyo bado haijathibitishwa.

Pia Jumuiya ya Wafanyakazi iliyoitisha maandamano hayo imedai kuwa kiongozi wake, Japhet Moyo amekamatwa kwa tuhuma za kuchochea wafanyakazi kushiriki katika maandamano.

Hata hivyo, hapo jana Mahakama Kuu Jijini Harare ilitoa uamuzi kuwa waziri wa serikali hana haki ya kuagiza kufungwa kwa mawasiliano ya internet.

WhatsApp yaweka zuio kutuma ujumbe zaidi ya mara tano
Tanzania ya zamani ilikuwa ikiishi kama nchi yenye Laana- Askofu Kakobe