Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa watu ambao wanasema elimu imeshuka nchini wanakosea kwani kuna sehemu ambazo elimu inaonekana ipo vizuri akitolea mfano wa chuo cha kilimo cha Sokoine University of Agriculture (SUA).

Ameyasema hayo wakati akiwa katika ziara yake mkoani Morogoro na kusema kuwa watu wasiseme kwa ujumla kushuka kwa elimu ili hali kuna sehemu watu wanafanya vizuri katika elimu, na kudai kuwa SUA wameweza kufundisha mpaka Panya na akaelewa hivyo ni wazi kuwa wapo vizuri sana.

“Unajua hata watu ambao wanasema elimu imeshuka sijui kama wamefika hapa kwa sababu wangefika hapa na kumuona Panya anajua bomu liko wapi nadhani asingesema elimu imeshuka, wanamuona Panya amefundishwa mpaka akaelewa eti binadamu ndiyo asielewe, mjue walimu wa hapa wanafundisha mpaka Panya siyo binadamu tu, mpaka anaelewa akinusa hapa kuna kifua kikuu,”amesema Rais Dkt. Magufuli 

Amesema kuwa walimu wa SUA na wanafunzi wapo vizuri sana katika masuala ya shule ndiyo maana wanaweza kufanya gunduzi mbalimbali ambazo zinatija na msaada katika maisha ya kila siku.

Aidha, Rais Magufuli amekiri kuwa katika awamu yake ya tano wamekuja na elimu bure na kusema kuwa huenda baadae ikaja kuwa na madhara ila itasaidia kuondoa ujinga kwa watu wengi ambao walikuwa wakikosa elimu hiyo kwa sababu ya kukosa ada ya kulipa shule.

Hata hivyo, Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa miezi kadhaa iliyopita aliwahi kusikika akisema kuwa kuna haja ya kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu elimu ya Tanzania kwa madai kuwa kuna unadhaifu mkubwa na kushuka kwa kiwango cha elimu ya Tanzania.

 

Maktaba yazuia vimini kupunguza wanaume kufeli
UNHCR vyuma vyakaza, wafadhili wakunja mikono