Bilionea ambaye ni mwanahisa mkuu wa Klabu ya Simba, Mohammed Dewji amefanya mazungumzo na Kocha wa timu hiyo, Mbelgiji Patrick Aussems siku moja baada ya kufanikisha kutinga katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.

Mo ambaye tangu juzi Simba ilipoipiga AS Vita 2-1 alikuwa akiweka sentensi fupi za kumshukuru Mungu na kufanya ibada, amefunguka kwa urefu kupitia Instagram akiweka picha inayomuonesha akiwa na Kocha Aussems aliyemtembelea.

“Huu ni ushindi wetu sote! Jana tumeandika historia kuwa klabu pekee Tanzania na Afrika Mashariki kuingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu huu. Nawapongeza na kuwashukuru wachezaji, benchi la ufundi, viongozi, wanachama, mashabiki, na wapenzi wote wa SIMBA! 🙏🏽 Safari inaendelea! Tuendeleze mshikamano wetu ili tufikie lengo letu la kuwa mabingwa wa Afrika, Insha’Allah. Asante Kocha Aussems kwa kunitembelea leo!” Ameandika Mo.


Simba imefikia lengo lililokuwa limetangazwa na Mo Dewji la kutinga katika hatua ya robo fainali ambapo imeishangaza Afrika kwa jinsi ilivyotoka kwenye maumivu ya vipigo viwili vya 5-0 na kuruka kiunzi kizito dhidi ya AS Vita ilikuwa miongoni mwa timu zilizowaadhibu vikali wana Msimbazi.

“Kwa Simba na kwa Tanzania ni kitu kizuri, lengo lilikuwa kufika katika hatua ya robo fainali. Unaweza kushangaa, sisi tulikuwa timu ambayo ilifungwa 5-0 mara mbili, lakini tumefanikiwa kuvuka. Hii inapaswa kuwa furaha kwa soka la Afrika Mashariki,” alisema Aussems muda mfupi baada ya mchezo wa juzi kati ya timu hizo uliofanyika ndani ya Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba imemaliza hatua ya 16 bora ikishika nafasi ya pili kwenye kundi D ikiwa na alama 9 nyuma ya Al Ahly yenye alama 10. Klabu hizo mbili ndizo zilizopenya kwenye kundi lao.

Sasa lengo limepandishwa ngazi hadi hatua ya nusu fainali ili kuweka historia mpya, ikiwa miaka takribani 25 iliyopita Simba walifanikiwa pia kutinga katika hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.

 

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Machi 18, 2019
Mwanasheria ampiga risasi wakitoka kanisani

Comments

comments