Bilionea Mohammed Dewji, aliyetekwa Alhamisi hii jijini Dar es Salaam amelifanya tukio hilo kuwa la kwanza kwa bilionea Afrika Mashariki, lakini sio la kwanza barani Afrika.

Mo alitekwa na watu wasiojulikana, ambao kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ni raia wa kigeni (wazungu).

Aidha, kumbukumbu zinaonesha kuwa tukio la Mo Dewji lina mfanano na matukio mengine matano ya utekaji wa mabilionea yaliyowahi kushuhudiwa mwaka huu nchini Afrika Kusini, Msumbiji na Nigeria.

Mapema mwezi Machi mwaka huu, bilionea Shiraz Gathoo alitekwa katika tukio ambalo watekaji wake walitengeneza kizuizi feki cha polisi na kulisimamisha gari alilokuwemo.

Gathoo aliachiwa na watekaji hao miezi mitano baadaye lakini taarifa za kuachiwa kwake hazikuwekwa wazi sana ikiwa ni pamoja na namna alivyoachiwa, huku baadhi ya vyombo vya habari vikidai kuwa watekaji walilipwa ‘kitita’ cha fedha.

Mwezi huohuo (Machi mwaka huu), bilionea mwingine ambaye ni mfanyabiashara wa Afrika Kusini, ambaye anafanya shughuli zake nyingi nchini Msumbiji, Andre Hanekom alitekwa akiwa kwenye eneo la kuegesha magari katika hotel ya kifahari ya Amarula, iliyoko jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji.

Aliachiwa baadaye na kulazwa hospitalini kwa muda, huku sababu za kutekwa kwake zikiwa kitendawili kwani kulikuwa na tetesi nyingi za kiusalama na ugaidi.

Andre Hanekom (kulia)

Bilionea mwingine ni Liyaqat Ali Parker, alitekwa katika eneo la kampuni yake jijini Cape Town nchini Afrika Kusini, Julai mwaka huu. Bilionea huyo ndiye mwanzilishi wa kampuni ya usambazaji wa chakula ya Foodprop Group.

Jeshi la polisi lilieleza kuwa Parker alitekwa na watu watano ambao walikuwa wanalifuatilia gari lake, walinzi wa eneo hilo walitishiwa kupigwa risasi na simu zao zote zilichukuliwa na watekaji.

Mwezi huohuo, baba yake Mikel Obi, mchezaji wa Timu ya Taifa ya Nigeria, aitwaye Chief Michael Obi alitekwa na watu wasiojulikana saa chache kabla ya kushuhudiwa mtanange wa kombe la dunia kati ya Nigeria na Argentina.

Mikel Obi (kulia) na baba yake Chief Obi

Chief Obi alitekwa Kusini-Mashariki mwa Nigeria, akiwa kwenye msafara wa msiba akitokea Jos, katika njia panda ya Makurdi-Enugu. Polisi walithibitisha kuachiwa kwake wiki moja baadaye, lakini mwanaye alisema kuwa watekaji walimtesa.

Tajiri mwingine aliyetekwa mwaka huu ni Sikhumbuzo Mjwara, mmiliki wa makampuni ya Mhlanga’s upmarket Barrio Restaurant. Alitekwa Agosti 30 mwaka huu nchini Afrika Kusini na watu wasiojulikana. Alitekwa nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Verulam, karibu na jiji la Durban.

Mjwara ni tajiri anayemiliki mtandao mkubwa wa biashara za madini, mitindo ya nguo na mengine.

Katika matukio hayo, waliopatikana baada ya kutekwa hawakuwa tayari kuelezea kilichowasibu na hata kuachiwa kwao.

Tuendelee kumuombea Mo Dewji, kijana mpambanaji aliyeiweka Tanzania kwenye rekodi ya Forbes kwa ukwasi wa ($1.5 bilioni), apatikane haraka akiwa salama.

Viongozi wa vyama vya ushirika watiwa mbaroni
Video: Msaidizi wa Mwalimu afichua siri, Maswali yenye utata kutekwa kwa Mo Dewji

Comments

comments