Menyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba, Mohammed Dewji amesema kuwa ujenzi wa uwanja wa Bunju katika awamu ya kwanza, ataugharamikia yeye mwenyewe.

Mo Dewji ameyasema hayo hii leo jijini Dar es salaam wakati wa uwekaji wa Jiwe la Msingi katika ujenzi huo, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe.

”Mimi kama mwanachama na shabiki wa Simba nimeamua kutoa pesa zangu mfukoni kwaajili ya ujenzi wa awamu ya kwanza ya Bunju Complex, na hizi hazihusiani na zile tulizokubaliana kwenye uwekezaji,” amesema Mo Dewji.

Kwa upande wake Waziri, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa wanasimba na vilabu vingine wanatakiwa kuendelea na zoezi la uwekezaji huku kanuni zikiendelea kuandaliwa na hakuna atakayekiuka.

”Timu ya Simba SC waliniomba waendelee nikawakubalia wakati ambao tunatengeneza kanuni na niwahakikishie zitafuatwa na zisitumike kuharibu hamasa, hata kwenye timu zingine karibuni muwekeze,” amesema Dkt. Mwakyembe.

Hata hivyo, Dkt. Mwakyembe amewataka wanachama na wafuasi wa klabu ya simba kuwaunga mkono viongozi wao pamoja na juhudi zote za ujenzi wa uwanja wa Bunju Complex hata kama hawana pesa za kutosha wanaweza kujitolea kwa kazi zinazohitaji nguvu ili kukamilisha jambo hilo la kihistoria.

Muhimbili yakanusha taarifa za uwepo wa mtu anayesadikiwa kuwa ni mchawi Wodini
Kabendera asomewa mashtaka matatu, moja la utakatishaji fedha