Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba Mohamed Dewji ‘Mo’ amesema yuko tayari kutoa ushirikiano na Mabingwa wapya wa Ligi Kuu Soka Visiwani Zanzibar klabu ya KMKM ili iweze kufanya vizuri katika mashindano ya Kombe la Klabu Bingwa Barani Afrika msimu ujao.

‘Mo’ amesema hayo alipoitembelea klabu ya Timu hiyo Maisara Mjini Unguja ambapo amesema ujio wake utafanikisha timu hiyo kupiga hatua zaidi ukilinganisha na awali.

Kauli hiyo ya Moo imekuja baada ya Mkuu wa KMKM Commodore Azana Hassan Msingiri kumuomba Mwekezaji huyo kuisadia timu yao ambao ndio wawakilishi wa Zanzibar katika Mashindano ya Kombe la Klabu Bingwa Barani Afrika kwa msimu wa mwaka 2021-2022.

Katibu Mkuu wa klabu ya KMKM Sheha Mohamed Ali amesema ni ndoto waliyokuwa nayo muda mrefu yakupata mfadhili anaejua thamani ya michezo na kuahidi kushirikiana nae kwa lengo la kukuza michezo Visiwani Zanzibar.

KMKM wametwaa Ubingwa wa Zanzibar msimu huu wa mwaka 2020-2021 baada ya kucheza michezo 22 ya Ligi na kufanikiwa kushinda michezo 13, sare 5 huku wakifungwa 4 na kupelekea kutwaa taji hilo wakiwa na jumla ya alama 44.

Makala: Kwanini leo ni siku ya Mtoto wa Afrika?
Simba SC kuifuata Polisi Tanzania