Mshambuliaji kutoka nchini Misri na Klabu ya Liverpool, Mohamed Salah amenyakuwa tuzo ya BBC ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Afrika ikiwa ni mwaka wa pili mfululizo.

Mo mwenye umri wa miaka 26 amepewa mapenzi tele na wapiga kura kwenye tuzo hiyo akiwapiku Medhi Benatia, Kalidou Koulibaly, Sadio Mane na Thomas Partey waliokuwa wanawania tuzo hiyo.

Kutokana na ushindi huo kutoka kwa mashabiki, Salah anakuwa mchezaji wa pili katika historia ya tuzo hizo kushinda tuzo hizo mara mbili mfululizo akiwa na rekodi sawa na Jay Jay Okocha wa Nigeria.

Mo Salah katika picha ya 2017 na 2018, akibeba tuzo ya BBC ya Mchezaji Bora wa Mwaka Afrika

Okocha alishinda mwaka 2003 na mwaka 2004, alipokuwa akiichezea timu yake ya taifa ya Nigeria pamoja na klabu ya Bolton. Mwaka huu, BBC imepokea kura 650,000 ikiwa ni idadi kubwa zaidi pia.

Mchezaji huyo wa mwaka wa Ligi Kuu ya Uingereza, amepata mafanikio katika klabu yake ya Liverpool akiifungia magoli 44 kwenye michezo 52 katika msimu uliopita.

“Nimepata hisia nzuri kushinda tena. Nimefurahi sana na kwakweli ningependa kushinda tena mwaka ujao,” alisema Mo Salah.

Mbali na mafanikio makubwa aliyoyapata kwenye Ligi ya Mabingwa, Salah alifanikiwa kuifungia timu yake ya Taifa magoli mawili kwenye Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika mwaka huu nchini Urusi. Ingawa Misri haikufanya vizuri kama wengi walivyotarajia kwenye fainali hizo, iliweka historia ya kuingia kwenye michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1990.

Salah amesema kuwa lengo lake ni kuhakikisha kuwa anaisaidia timu yake ya Liverpool kushinda kikombe kizito mwaka 2019 ili kuwapa furaha zaidi mashabiki.

 

Jaji Mkuu aeleza Kiingereza kinavyowapa tabu mawakili
Kama bado nina nguvu, sitarajii kung'oka madarakani- Museveni

Comments

comments